Home LOCAL TAFITI MAZAO YA MISITU KUONGEZA KIPATO KWA WANANCHI

TAFITI MAZAO YA MISITU KUONGEZA KIPATO KWA WANANCHI

Na Farida  Mangube,MOROGORO

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hapa nchini imezitaka taasisi za utafiti na zile zinazotoa mafunzo ya misitu kuendelea kubuni mbinu na teknolojia rahisi kwa ajili ya wananchi wa vijijini wenye ujuzi na mitaji midogo ili kuwawezesha kutumia ipasavyo rasilimali za misitu kwa njia endelevu na yenye manufaa kwa taifa na vizazi vijavyo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (Mb) kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya utoaji wa taaluma ya misitu katika Chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo yaliyofanyika katika Chuo hicho ambapo alisema kuwa SUA ione umuhimu wa kuwa na mikakati thabiti ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Mhe. Kipanga alisema kuwa nafasi ya sekta ya misitu katika maisha ya binadamu na katika maendeleo ya taifa la Tanzania ni kubwa kama ambavyo utafiti unavyoeleza kuwa eneo la misitu kwa Tanzania ni takribani hekta milioni arobaini na nane ambalo ni sawa na asilimia hamsini na tano za ardhi yote ya Tanzania bara

Rasilimali za misitu zinatoa fursa ya ajira kwa watanzania na wasio kuwa Watanzania zaidi ya milioni tatu, upatikanaji wa maji, makazi na malisho ya wanyamapori, uhifadhi wa udongo na baianowai, urutubishaji wa hewa ukaa pamoja na maendeleo ya utalii wa kiikolojia” Naibu waziri Kipanga alisema.

Hata hivyo amesema kuwa umuhimu wa sekta ya misitu huonekana pia katika maeneo yaliyoainishwa mpango wa maendeleo ya taifa na maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa ambapo alisema kuwa katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa kitivo cha Mafunzo ya Misitu,Wanyamapori na Utalii hapa SUA. Wataalamu wa misitu 2630 wamehitimu mafunzo hayo kwa ngazi mbalimbali ambao wanasimamia rasilimali za misitu ndani na nje ya taifa la Tanzania.

Kwa hapa nchini wataalamu hawa wamewezesha kutengwa kwa hekta milioni arobaini na nane nukta moja (48,100,000 ha) ya hifadhi za misitu pamoja na uanzishwaji wa hekta laki tano themanini na mbili elfu na mia saba ishirini na tisa (582,729 ha) za mashamba ya misitu ya kibiashara” Naibu waziri Kipanga alisema.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo, Prof. Raphael Chibunda alieleza kuwa Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na wafanyakazi wa kitivo cha misitu kuwa wanakitazama kitivo hicho kwa jicho la kipekee na mikakati ya kukifanya kuwa kitivo cha umahiri kutokana na SUA kuwa Chuo kiongozi kwenye sekta ya misitu katika ukanda wa SADC na nchi za Afrika Mashariki.

Kupitia maadhimisho hayo, Menejimenti na Wafanyakazi tuna kila sababu ya kujitathmini juu ya sekta ya misitu na namna ya kudhibiti uharibifu wa misitu na namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi” Prof. Chibunda alisema.

Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala alisema, kuwa upekee wa taaluma ya misitu inayotokana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo taifa la Tanzania pamoja na mataifa mengine yameshuhudia matokeo makubwa katika sekta ya misitu yaliyotokana na uwepo wa kitivo cha misitu katika Chuo hicho.

Hata hivyo amewataka vijana na wataalamu waliosoma katika Chuo hicho na watanzania kwa ujumla kuenzi jitihada za waasisi wa Chuo hicho akiwemo Hayati Edward Moringe Sokoine, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na waasisi wengine.

Previous articleHALI YA LISHE NCHINI INAENDELEA KUIMARIKA” DKT. YONAZI
Next articleMME WANGU AKIENDA NJE HAWEZI, ILA KWANGU MAMBO NI MOTO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here