Home LOCAL SIERRA LEONE YAIPONGEZA TARURA UJENZI WA MADARAJA NA BARABARA ZA MAWE

SIERRA LEONE YAIPONGEZA TARURA UJENZI WA MADARAJA NA BARABARA ZA MAWE

#Matumizi ya mawe kupunguza gharama zaidi ya 40%

#Ushirikishwaji wa vikundi vya kijamii kusaidia kulinda miundombinu

Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Matengenezo ya Barabara wa Sierra Leone Bw. Mohamed Kallon ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa madaraja na barabara kwa kutumia mawe.

Akizungumza na waandishi wa habari Mtendaji Mkuu huyo amesema wamefurahishwa na teknolojia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inapunguza gharama za ujenzi pia kutumia malighafi zilizopo eneo husika.

Amesema kwamba ujio wao hapa nchini ni kujifunza ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya katika maeneo ya mipango,ushirikishwaji wa wananchi na utumiaji wa teknolojia mbadala.

“Wananchi wa Sierra Leone ni wazalishaji na wengi wanaishi vijijini hivyo kwa kutumia teknolojia ya mawe itawarahisishia kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda kwenye masoko”

Ameongeza kusema kuwa kati ya agenda tano za Rais wa nchi yao ni kuilisha Sierra Leone hivyo kitu muhimu ni kufungua barabara ili kuuza na kusafirisha mazao toka kwa wakulima.

Kwa upande wa ushirikishwaji wa wananchi (vikundi vya kijamii) amesema wameona ni fursa nzuri kuja kujifunza Tanzania kwa sababu wao hawaitumii njia hiyo ya vikundi vya kijamii ila tayari TARURA wamefanikiwa katika utekelezaji wa miradi yao kwenye wilaya.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema kwamba matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara kama mawe yaliyopo kwenye eneo la kazi inapunguza gharama za ujenzi wa madaraja na barabara kwa zaidi ya asilimia 40.

Kwa upande kwa ushirikishwaji wa vikundi vya kijamii kwenye ujenzi na matengezo ya barabara Mhandisi Seff amesema kupitia mradi wa uboreshaji wa barabara za vijijini ambao ni mkopo rahisi toka Benki ya dunia ambao wanasaidia kuanzisha, kufundisha na kuviwezesha vikundi hivyo kufanya kazi za matengenezo ya barabara kwa weledi na umakini.

“Faida kubwa ya kuvitumia vikundi hivyo inapunguza gharama kwani vinatoka maeneo yale yale zinapopita barabara pia inasaidia kulinda miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani kwani wanatambua barabara ni mali yao”.

Hata hivyo Mhandisi Seff aliongeza kusema kuwa wao kama TARURA wapo tayari kushirikiana na Sierra Leone kwa kuwapatia wataalam wa kufundisha pale panapohitajika.

Timu ya Viongozi na wataalam kutoka Sierra Leone wapo nchini kwa ajili ya kujifunza ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya katika maeneo ya mipango, ushirikishwaji wa wananchi pamoja na teknolojia mbadala na wanatarajia kuvitembelea baadhi ya vikundi vya kijamii Mkoani Njombe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here