Home BUSINESS RC SHIGELLA; BoT IMEWEKA UTARATIBU MZURI KUNUNUA DHAHABU

RC SHIGELLA; BoT IMEWEKA UTARATIBU MZURI KUNUNUA DHAHABU

 
Na: Hughes Dugilo, Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella, amesema kuwa Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, wakati na wakubwa, na kwamba matunda yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu kwenye Taifa hususani  mkoa wa Geita yaweze kuwasaidia watanzania.

Shigella ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia maonesho ya saba ya Teknolojia katika sekta ya madini yanayotarajiwa kufunguliwa rasmi Oktoba 5, 2024 katika viwanja vya EPZ , Bombambili Mkoani Geita.

Amesema kuwa Bunge lililomalizika la Bajeti, miongoni mwa Sheria zilizotungwa ni pamoja na Sheria ambayo ilielekeza asilimia 20 ya uzalishaji wa Dhahabu inununuliwe na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), nakwamba dhamira ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Taifa linakuwa na hifadhi ya Dhahabu badala ya fedha za kigeni.

‘Kama unavyofahamu mwaka jana kilo moja ya Dhahabu ilikuwa inauzwa Dola elfu 50, leo kilo moja imekwenda mpaka Dola elfu 70 sasa haya mabadiliko tungekuwa tunahifadhi Dhahabu yetu ingekuwa na thamani kubwa kuliko kuhifadhi fedha za kigeni.

‘Ninawaomba na kuwasihi watanzania hususani wafanyabiasha wa Dhahabu waielewe Sheria hii, na bahati nzuri Benki Kuu, ilitoa utaratibu wa namna ya kununua Dhahabu, na zuri zaidi ina punguzo kubwa sana la tozo na kodi ambazo zinatolewa na Serikali,  lakini bei walioitoa ni nzuri kuliko hata ile wanayokwenda kuuza kwenye maeneo mengine’ amesema Shigella.

Ameongeza kuwa kwa sasa kuna wafanyabiasha wa Dhahabu ambao baadhi yao wameitwa Dodoma ambapo  mazungumzo kati yao na Wizara ya Madini, pamoja na Tume ya Madini yanaendelea, nakwamba wengine wameendelea na biashara baada ya Serikali na Benki Kuu kutoa utaratibu.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyabiasha na wachimbaji Wadogo, wakati na wakubwa, kuendelea kufanya Biashara na Benki Kuu katika utaratibu uliopo ambao umetoa unafuu mkubwa wa bei ukilinganisha na maeneo mengine waliyokuwa wakipeleka dhahabu zao kuuza.

Mnamo octoba 1, 2024 Benki Kuu ya Tanzania BoT, ilitoa ilitoa taarifa ya Mpango wa ununzi wa Dhahabu nchini iliyolenga kutoa fursa kwa wauzaji wa Dhahabu kuuza Dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa bei ya ushindani ya soko la kimataifa, ambapo chini ya mpango huo wauzaji wa dhahabu watapata punguzo la ada na uhakika wa malipo ya haraka wakiuza asilimia 20 ya Dhahabu zao Benki Kuu kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 59 cha sheria ya madini sura ya 123.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here