Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akipata maelezo kutoka kwa Afisa Habari wa TASAF, Meleckzedeck Nduye wakati alipotembelea kwenye banda hilo katika ufunguzi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yenye kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi” yanayofanyika katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.
……………..
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi wakati wa Wiki ya Huduma za Fedha inayoendelea jijini Mbeya.
Akizungumza wakati alipotembelea katika banda la TASAF na kuona shughuli mbalimbali za walengwa, Profesa Mkenda alisifu juhudi za TASAF za kusaidia familia zenye kipato cha chini kupitia miradi mbalimbali ya kijamii inayolenga kuinua hali za maisha ya wananchi.
Profesa Mkenda alieleza kuwa, kupitia TASAF, jamii nyingi zimeweza kunufaika na fursa za kiuchumi, elimu, na huduma za afya, na hivyo kuwasaidia kuwa na uwezo wa kujitegemea. Alihamasisha wananchi kuendelea kutumia fursa zinazotolewa na mfuko huo ili kuboresha hali zao za maisha.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa elimu ya kifedha kwa wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini, ambapo TASAF imekuwa ikitoa msaada wa moja kwa moja kwa kaya maskini kupitia programu za kupunguza umaskini na kuongeza ustawi wa kijamii.
Katika maelezo yake, Profesa Mkenda pia aliipongeza TASAF kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya fedha na kujua umuhimu wa kujiwekea akiba, pamoja na kupata mikopo yenye masharti nafuu.
Maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha yamewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya kifedha, wakiwemo benki, vikundi vya SACCOS, na mashirika yasiyo ya kiserikali, ili kutoa elimu na huduma zinazohusu masuala ya fedha kwa wananchi.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akipata maelezo kuhusu shughuli za ujasiriamali walizofundishwa na kuwezeshwa na TASAF kutoka kwa Kisa Lauden wa kikundi cha Amkeni cha Ghana Magaribi jinini Mbeya wakati alipotemnelea kwenye banda hilo katika ufunguzi wa wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yenye kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi”yanayofungua katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya
Wannanchi mbalimbali wakipata maelezo kutoka kwa maofisa wa TASAF wakati w alipotembelea kwenye banda hilo.