Home BUSINESS NHC YAJITANUA KIBIASHARA KATIKA MIKOA

NHC YAJITANUA KIBIASHARA KATIKA MIKOA

Muonekano wa jengo la Mtanda Plaza lililopo Matanda mkoani Lindi ambapo ujenzi wake unaendelea. Hili ni jengo kubwa na lakisasa lenye kutoa huduma zote sehemu moja (one stop centre) zikiwamo benki, migahawa, Ofisi na maduka.

Na; Mwandishi wetu.

Katika kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kukua kadri siku zinavyosonga mbele na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuhakikisha wafanyabiashara wanapata sehemu bora za kufanyia biashara zao, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeongeza kasi ya kujenga majengo mengi ya biashara katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Majengo hayo yameleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara kutokana na kuwapatia fursa wafanyabishara kupata maeneo ya kisasa na bora ya kufanyia biashara na kukidhi mahitaji makubwa yaliyokuwa yakiwakabili.

Kwa sasa Shirika la Nyumba la Taifa limekuja na miradi mingi ya majengo ya biashara lengo likiwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wanapata sehemu nzuri za kufanya biashara zao lakini pia kuhakikisha wafanyabishara hawa na wajasiriamali wanafikia ndoto zao.

Miradi hii imekwishaanza kutekelezwa kwenye baadhi ya Mikoa na inakwenda kwa kasi kubwa ili kuhakikisha walengwa wanatimiza ndoto zao kwa kupatiwa maeneo muhimu ya kujipatia kipato lakini pia kuinua uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa linajengwa na NHC eneo la Mtanda Lindi kwa ajili ya Ofisi na shughuli za kiabiashara. Anayetoa maelezo kwa Mkurugenzi Mkuu ni Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC QS Dkt Godwin Maro na pia yupo Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi Bw. Omari Makalamangi.

Katika Mikoa hiyo, tayari NHC ina majengo ya biashara lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa majengo hayo ndipo Shirika likaona ipo haja ya kuongeza maduka mengine na hivyo kuwasaidia wafanyabiashara kupata maeneo mazuri, makubwa na yenye huduma zote za kijamii.

Moja ya majengo hayo ambayo uwepo wake utawasaidia hata wananchi kwa kiasi kikubwa ni Mtanda Plaza – Lindi ambalo ni jengo kubwa la kisasa lenye kutoa huduma zote sehemu moja (one stop centre) zikiwamo benki, migahawa, Ofisi na maduka. Ujio wa jengo hili utatoa unafuu kwa wananchi wa Lindi na Mikoa ya jirani na hata wageni kutoka nchi jirani ya Msumbiji kuweka vitegauchumi vyao pale. 

Hili ni moja ya jengo kati ya mengi yanayojengwa na NHC hapa nchini na hii yote ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wafanyabishara na wajasiriamali wanafanya shughuli zaidi kwa weledi mkubwa.

Majengo mengine mfanano na hilo yanajengwa katika Mkoa wa Singida ambapo jengo litakalojulikana kama Singida 2F maaandalizi ya kulijenga yamepamba moto nah ii itaongeza idadi ya majengo kama hilo baada ya lile la ghorofa moja lijulikanayo kama Singida Shops na Singidani Complex yaliyokwishajengwa hapo awali. Uwepo wa majengo haya umelisukuma Shirika la Nyumba la Taifa kuja na jengo lingine la Singida 2F baada ya wafanyabisha kuchangamkia fursa hiyo katika majengo ya awali na wengine kuonekana kukosa. 

Mchango wa NHC katika majengo haya makubwa ya biashara umekuja kivingine kwa lengo la kuendelea kutoa mchango wake katika sekta ya biashara ambapo sasa majengo makubwa yanajengwa katika Mikoa mbalimbali. Eneo linguine yanakojengwa maduka haya ni Mount Meru Plaza Kibla – Arusha, Tabora Complex -Tabora, Mkwakwani Plaza – Tanga, Plot 35/J Sokoine Arusha, Iringa Project (ICC) na Plot 38/E Joel Maeda Arusha. 

Ujio wa majengo haya ni faraja kubwa kwa wafanyabishara ambapo kwa muda mrefu wamekuwa na kiu kubwa ya kutaka kuendeleza biashara zao katika maduka makubwa, yenye nafasi na miundombinu rafiki katikati ya miji yetu.

Muonekano wa jengo la maduka ya Biashara katika mji wa Masasi  – Masasi Complex. 

NHC pia inatekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya biashara katika miji mikubwa kibiashara kama Dar es Salaam – Kariakoo, Morogoro, Masasi, Kahama na Bukoba. Miradi hii inalenga kutoa nafasi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa ndani kuanzisha na kuendesha biashara zao katika mazingira bora na rafiki. 

Kwa mfano, Kariakoo Plaza na jengo litakalojengwa Lumumba Street, Morogoro yanatarajiwa kuwa kitovu cha biashara, yakitoa nafasi kwa wafanyabiashara wa ndani na nje kuanzisha biashara zao, hivyo kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa maeneo hayo.

Kwa wafanyabiashara wa Lindi, Lindi Commercial Complex inatoa fursa kwa maduka, ofisi na maeneo ya burudani, ikiwa ni sehemu ya mpango wa NHC kuimarisha mazingira ya kibiashara katika Mkoa wa Lindi. Vilevile, Masasi Plaza ni mradi unaolenga kuimarisha biashara na kutoa fursa mpya kwa wajasiriamali wa Masasi, ambao ni mji unaokua kwa kasi kibiashara ukanda wa Kusini mwa Tanzania. 

Nao mradi wa Kashozi Commercial Complex Manispaa ya Bukoba, unaleta matumaini mapya kwa wafanyabiashara wa Bukoba na nchi jirani. Ya kuwa na fursa za kufanya uwekezaji.

Haya yote ni sehemu ya mpango wa NHC kuhakikisha kuwa maeneo yote ya Tanzania yanashiriki katika maendeleo ya kiuchumi kwa kuongeza wigo wa kibiashara.

Sehemu ya muonekano wa mgahawa uliopo katika jengo la Biashara la Bukondamoyo Kahama, baada ya kukamilika ujenzi wake.

NHC pia inaendelea kukamilisha mradi wa ujenzi wa maduka 50 katika eneo la Bukondamoyo, Kahama ambao nao ni kitovu cha biashara maduka ambayo yatawasaidia  kwa lengo wajasiriamali wadogo kuanzisha biashara zao na kutoa huduma kwa wakazi wa mji huo wa kibiashara. Mradi huu unalenga kuongeza nafasi za biashara na kukuza kipato cha wajasiriamali wadogo, hivyo kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Kahama na maeneo ya jirani.

Hizi ni fursa muhimu kwa NHC katika kutoa huduma zake kwa wadau wa sekta ya mbalimbali na ni nafasi ya pekee kwa wananchi kufahamu namna NHC inavyotekeleza miradi yake kwa weledi na ubunifu ili kuboresha maisha ya watu na uchumi wa Taifa.

Kwa kuwekeza katika majengo ya makazi na biashara, NHC inasaidia kuboresha maisha ya Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla. Wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hizi za kipekee zinazotolewa na NHC, kwa kuwa ni hatua muhimu kuelekea kwenye Tanzania yenye maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wote.

NHC na Maendeleo Endelevu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here