Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa hatua ya kuanzisha utaratibu wa kuweka akiba ya dhahabu, hatua ambayo ina lengo la kusaidia kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania wakati wa misukosuko ya kiuchumi.
Akizungumza leo, Oktoba 5, 2024, wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya EPZ Bombambili, Mkoani Geita, Dkt. Biteko ameisifu Wizara ya Madini kwa kazi nzuri ya kuweka akiba ya dhahabu kupitia BoT na kuhimiza wachimbaji kuuza dhahabu kwa Benki hiyo kwa bei rafiki.
Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa wachimbaji wa madini kuwa na akiba ya dhahabu, kwani itasaidia si tu kuimarisha shilingi ya Tanzania, bali pia kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta hiyo.
BoT inatekeleza mpango wa ununuzi wa dhahabu, ikitoa fursa kwa wauzaji kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu kwa bei ya ushindani wa soko la kimataifa. Mpango huu pia unatoa punguzo la ada na uhakika wa malipo ya haraka kwa wauzaji watakaouza asilimia 20 ya dhahabu zao kwa Benki Kuu, kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Madini Sura ya 123.
Ameeleza kuwa maonesho hayo yanawapa fursa taasisi mbalimbali, vyama vya madini, mashirika ya kimataifa, na asasi za kiraia kubadilishana ujuzi na uzoefu. Hii itawasaidia wadau katika mnyororo wa thamani ya madini, na kufanya maonesho kuwa bora kila mwaka, huku wadau wengi wakivutiwa kuja kujifunza.
“Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini,” amesema Dkt. Biteko. Pia amewaalika wadau wenye nia njema kuwekeza nchini kwa kutafuta maeneo ya uchimbaji na kuongeza thamani ya madini, jambo ambalo litakuza fursa za ajira.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 118 kwa ajili ya kupeleka umeme kwa wachimbaji wadogo wa madini, ambapo kwa Mkoa wa Geita pekee wametenga shilingi bilioni 7.3.
Amehitimisha kwa kusema kuwa serikali itaboresha miundombinu katika maeneo ya uchimbaji ili kuhakikisha wachimbaji wanapata mazingira bora ya kufanya kazi na kuimarika zaidi.