Home BUSINESS MAMLAKA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA KEMIKALI

MAMLAKA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA KEMIKALI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Yasistiza matumizi salama ya Kemikali kwa Wachimbaji Katika Maonyesho ya 7 ya Teknolojia

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inashiriki kwenye Maonyesho ya 7 ya Teknolojia kwa malengo makuu manne, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya matumizi salama ya kemikali kwa wachimbaji na umma kwa ujumla. Mamlaka hiyo pia inatoa huduma moja kwa moja, kama vile usajili wa wadau na utoaji wa vibali, pamoja na kuelimisha umma kuhusu shughuli mbalimbali wanazofanya kama vile uchunguzi wa kimaabara na masuala yanayohusiana na jinai. Aidha, mamlaka hiyo inachunguza usalama wa vyakula na mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 7, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndio, wakati wa Maonyesho ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili, mjini Geita, alisema mamlaka hiyo ipo tayari kutoa huduma zote zilizokusudiwa kwa wananchi wa Geita.

“Tupo tayari kuwahudumia wananchi wa Geita kadiri ya uwezo wetu na wakati wote tutakapokuwa hapa. Huduma zote za usajili zitatolewa hapa,” alisema Ndio.

Pia, alitoa wito kwa wadau wa sekta ya madini kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi na salama ya kemikali, hasa kwa wachimbaji wa madini kama dhahabu, ambapo kemikali zinazotumika ni hatarishi.

“Tunafahamu kuwa wachimbaji, hasa wa dhahabu, wanahitaji kutumia kemikali ili kupata dhahabu. Baadhi ya kemikali hizi ni sumu, lakini zinahitajika katika mchakato wa uzalishaji. Kwa sasa, wachimbaji bado wanatumia zebaki, na tunatafuta mbadala wake ili tuiondoe sokoni baada ya teknolojia mpya kupatikana. Hata hivyo, kwa sasa zebaki bado inatumika,” aliongeza Ndio.

Ndio aliwataka wachimbaji kuzingatia matumizi salama ya kemikali na kuhakikisha kila mtumiaji wa kemikali amesajiliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitatumika kwa wale watakaokiuka taratibu, ikiwemo kutozwa faini, lakini akasema lengo ni kuepusha hatua hizo kwa kuhakikisha kila mmoja anakidhi vigezo vinavyohitajika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here