Home LOCAL MAJALIWA ASHUHUDIA MADIWANI WA CUF, ACT WAZALENDO WAKIREJEA CCM

MAJALIWA ASHUHUDIA MADIWANI WA CUF, ACT WAZALENDO WAKIREJEA CCM

*_Yumo pia Katibu Kata wa CUF_*

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa mwishoni mwa wiki hii, ameshuhudia madiwani wawili na Katibu Kata kutoka vyama vya CUF na ACT-Wazalendo wakirejea Chama cha Mapinduzi.

Akiwa kwenye kijiji cha Milola katika siku ya kwanza ya ziara yake, Mheshimiwa Majaliwa alishuhudia madiwani wa Kata za Milola na Rutamba wakitambulishwa na Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye senta ya Milola, Kata ya Milola, Manispaa ya Lindi.

Viongozi waliorejea CCM ni Diwani wa Milola, Bw. Hussein Kimbyoko kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na Diwani wa Rutambi, Bw. Athumani Mmaije kutoka Chama cha ACT – Wazalendo.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake jimboni Ruangwa, Mheshimiwa Majaliwa alishuhudia wanachama wengine wawili wakikabidhi kadi zao kwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ruangwa, Mzee Ibrahim Issa Ndoro katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Wandorwa, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Wanachama hao ni Alhaji Abasi Abdallah Chinguwile kutoka ACT WAZALENDO ambaye alikuwa mwanachama katika kijiji cha Mmawa, Kata ya Likunja, wilaya ya Ruangwa. Mwingine ni Bw. Jafari Juma Nang’anda kutoka CUF ambaye pia alikuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi na Katibu Kata wa Kata ya Nachingwea, wilayani humo.

Akizungumza baada ya kupokewa na viongozi wa CCM, Bw. Jafari Nang’anda alisema ana imani na viongozi wa CCM wa mkoa na wilaya na akawaomba watambue kuwa anaweza kufanya kazi saa yoyote na mahali popote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here