Home BUSINESS MAADHIMISHO YA MIAKA 101 YA JAMHURI YA UTURUKI, TANZANIA YAJIVUNIA

MAADHIMISHO YA MIAKA 101 YA JAMHURI YA UTURUKI, TANZANIA YAJIVUNIA

• Mahusiano kati ya Tanzania na Uturuki yazidi kuimarika

Na Happiness Shayo-Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema kuwa ikiwa leo ni maadhimisho ya miaka 101 ya Jamhuri ya Uturuki, mahusiano ya kidiplomasia kati yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yamezidi kuimarika katika maeneo ya biashara, miundombinu , utalii na elimu.

Ameyasema hayo leo Oktoba 29,2024 katika Maadhimisho ya Miaka 101 Tangu Kutangazwa kwa Jamhuri ya Uturuki yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Tanzania na Uturuki zimedumisha uhusiano wa kiuchumi kwenye mahusiano ya kibiashara na uwekezaji, ambapo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, mauzo ya Tanzania kwenda Uturuki yalikuwa wastani wa dola milioni 15.9, wakati uagizaji kutoka Uturuki ulikuwa wastani wa dola za Kimarekani milioni 242.1” amesisitiza Mhe. Chana.

Ameongeza kuwa uwepo wa wawekezaji kutoka Uturuki nchini Tanzania, uanzishwaji wa miradi 106 iliyosajiliwa Tanzania Bara yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 414.23 na miradi 12 Zanzibar yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 96.4, kwa pamoja ikizalisha karibu ajira 6,800 vyote vinaonyesha uimara wa mashirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo kati yake na Uturuki katika sekta ya utalii, ulioimarishwa na kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ambapo imekuwa chachu katika kuchangia ongezeko kubwa la idadi ya watalii wa Kituruki wanaotembelea Tanzania, kutoka wageni 5,177 mwaka 2020 hadi 11,203 mwaka 2023.

Naye, Balozi wa Jamhuri ya Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Mehmet Güllüoğlu, amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mazingira ya biashara na uwekezaji yameboreshwa hivyo kupelekea kuanzishwa kwa kampuni za Kituruki zaidi ya 200 nchini Tanzania.

Amesema maadhimisho hayo ni mwanzo mzuri wa kuyaboresha mahusiano kati ya Tanzania na Uturuki katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu, utalii na biashara.

Uhusiano wa Kidiplomasia katika Tanzania na Uturuki ulianza tarehe 5 Julai, 1963 na umekuwa na manufaa kwa pande zote.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), Waheshimiwa Mabalozi na Makamishna Wakuu, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Serikali na Maafisa wa Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here