Home BUSINESS KONGANI LA VIWANDA VYA KUBANGUA KOROSHO MBIONI KUJENGWA MTWARA

KONGANI LA VIWANDA VYA KUBANGUA KOROSHO MBIONI KUJENGWA MTWARA

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameipongeza Bodi ya Korosho kwa hatua ya kimkakati ya kuwakomboa wakulima kiuchumi njiani Mtwara kwa kuanza ujenzi wa Kongani ya Viwanda vya Kubangua Korosho.

Amezitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi huo tarehe 1 Oktoba 2024 ambapo Bw. Francis Alfred, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho alieleza ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.

Bw. Francis aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi imeanza kwa gharama za shilingi bilioni 7.5 zitakazogharamia umeme, maji, ujenzi wa maghala mawili kila mojawapo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za bidhaa, fensi ya kuzungusha eneo lote la ekari 1572, barabara za ndani zenye urefu wa kilometa 11, mageti 3.

Aidha, ujenzi mwingine utahusisha viwanda 30 vya kubangua Korosho, kuchakata ufuta, mbaazi na mazao mengine.

“Nimeridhishwa na kazi inayoendelea na nitoe rai ifikapo mwezi Oktoba 2025 tuwe tayari na kiwanda kimoja cha kuanza kubangua korosho zenye uwezo wa tani 3000. Pia, nimepokea ombi la Mbunge Chikota la kujenga Zahanati, hivyo nayo itajengwa ndani ya mchakato wa mradi mzima,” amesema Waziri Bashe.

Waziri Bashe pia amesema Bodi ya Korosho imeajiri zaidi ya Maafisa Ugani 500 ambao pamoja na huduma za Ugani wakatakazotoa, pia watakaohusika na ugawaji wa pembejeo na ukusanyaji wa kanzidata sahihi za wakulima.

Mradi wote hadi kukamilika mwaka 2030 na viwanda vyote 30 na miuondombinu mingine utakuwa na gharama ya takribani shilingi bilioni 300.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here