Home BUSINESS KONGAMANO LA KWANZA LA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA NISHATI KUFANYIKA TANZANIA

KONGAMANO LA KWANZA LA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA NISHATI KUFANYIKA TANZANIA

Dar es Salaam, Tanzania – Mkutano wa kwanza wa Uwekezaji katika Sekta ya Nishati Tanzania unatarajiwa kufanyika tarehe 12-13 Novemba 2024 jijini Dar es Salaam, ukiungwa mkono na washirika muhimu kutoka sekta binafsi na serikali.
 
 Tukio hili la kihistoria linalenga kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya nishati kutoka Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, likiwa jukwaa la wadau kukuza mtandao, kubadilishana ujuzi, na kujadili mustakabali wa uwekezaji kwenye sekta ya nishati nchini.
Mkutano huu umeandaliwa kwa pamoja na HBZ International na Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC), na unakwenda sambamba na nafasi mpya ya Tanzania kama kitovu cha nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku ikiweka kipaumbele kwenye nishati safi na maendeleo endelevu. 
 
Kongamano hili linaungwa mkono na TANTRADE pamoja na taasisi nyingine za serikali zinazohusika, na ni hatua kubwa kwa sekta ya nishati nchini, kwani lengo lake ni kuonyesha fursa zinazochipukia za uwekezaji katika sekta hiyo. 
 
Bw. Herman Zaidin, Mkurugenzi Mtendaji wa HBZ International, amesema, “Kongamano hili limekuja kwa wakati muafaka kwa Tanzania, inapojipanga kimkakati kuwa kitovu thabiti cha nishati katika kanda ya Afrika Mashariki, ambayo itaifanya Affrika Mashariki kuwa na nafasi kubwa katika soko la kimataifa la nishati. Tunakaribisha wadau wote kuungana nasi katika tukio hili la kihistoria.”
 
Bw. Salim Baabde, Mkurugenzi wa Camel Oil (sehemu ya Amsons Group) na Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya TAOMAC, amesifu ujio wa kongamano hilo, akisema unafanyika wakati muafaka kwani nchi imejikita kuleta maendeleo chanya katika sekta ya nishati.
 
“Mkutano huu unafanyika wakati muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kampeni ya kukuza matumizi ya nishati safi kwa kupitisha Mkakati wa Kitaifa wa Kupika kwa Nishati Safi (2024-2034). Lengo kuu la mkakati huu ni kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi za kupikia ifikapo mwaka 2034. Tanzania pia imeshuhudia uzinduzi wa Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, wenye uwezo wa megawati 2,115. Hii ni fursa nzuri sana kwa uwekezaji katika sekta ya nishati ya Tanzania,” amesema Bw. Baabde.
 
Mkutano huo utajumuisha kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Kamati Maalum ya Kongamano, inayojumuisha wataalamu wenye uzoefu mkubwa wa sekta ya nishati, akiwemo Bw. Salim Baabde.
 
 Lengo ni kutoa uelewa wa kina kwa washiriki kuhusu mazingira ya kisheria na sera yanayoongoza sekta ya nishati nchini Tanzania na kujadili masuala muhimu yatakayochambuliwa kwa undani na wataalamu wa sekta hiyo. 
 
Washiriki watapata maarifa kuhusu mada muhimu kama fursa za uwekezaji, miradi mipya, suluhisho za nishati safi, mifumo ya kisheria, na mengine mengi.
 
Bw. Raphael Mgaya, Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC, amesisitiza umuhimu wa kongamano hilo kwa wadau wa sekta ya nishati: “Ni heshima yetu kuandaa kongamano hili kubwa. Tunaamini litakuwa jukwaa zuri kwa wadau wa nishati kukutana na kushirikiana na watunga sera, wafadhili, wasimamizi, wasambazaji, na wawekezaji. Washiriki wataweza kuelewa mazingira ya kisheria na sera yaliyopo Tanzania na vilevile kujifunza kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya nishati. Wanachama wetu na wasambazaji wengine watapata nafasi ya kuonyesha bidhaa na huduma zao kwa washiriki, hivyo kuboresha bishara zao,” amesema.
 
Mkutano huu unatarajiwa kuvutia wadau mbalimbali kutoka sekta ya nishati ya ndani ya Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki, wakiwemo watunga sera, wawekezaji, wasambazaji, na viongozi wa sekta hiyo. Kongamano hili litachangia kuimarisha ushirikiano na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya nishati ya Tanzania kwa kutoa jukwaa la wadau kuunganishwa na kubadilishana mawazo.
 
Mkutano wa Uwekezaji wa Nishati Tanzania unajitofautisha na mikutano mingine kwa kutoa ajenda iliyochambuliwa kwa kina na Kamati ya Kongamano, kuidhinishwa na wizara muhimu za serikali, na kuungwa mkono na ushirikiano wa kina wa vyombo vya habari. Tukio hili litatoa maarifa ya thamani kuhusu mazingira ya nishati yanayobadilika kwa kasi nchini Tanzania na juhudi za zinazolenga kuongeza matumizi ya nishati safi na mbadala.
 
Kuhusu Waandaaji
 
HBZ International, ni shirika la kimataifa la mawasiliano lenye zaidi ya miaka 10 ya uzoefu na miradi zaidi ya 300 iliyokamilishwa duniani kote. HBZ imeungana na TAOMAC, mdaui mkuu katika sekta ya nishati ya Tanzania, na wadau wengine wakubwa katika sekta hiyo ya nishati kuleta kuandaa kongamano hili muhimu.
 
Ili kujifunza zaidi kuhusu Kongamano la Uwekezaji wa Nishati Tanzania na kujisajili ili kushiriki, tafadhali tembelea https://teis2024.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here