Na WAF – Bungeni, Dodoma
Imetajwa kuwa kaya masikini zipatazo Milioni 1.2 nchini zitanufaika na mpango wa Serikali wa kusaidia kaya zisizojiweza ili ziweze kupata huduma za afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Oktoba 23, 2024 wakati akiwasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Elibariki Kingu.
Waziri Mhagama amesema Tanzania Bara ina jumla ya kaya Milioni 14.8 ambapo kaya Milioni 3.9 ni kaya zisizo na uwezo kati ya kaya hizo zisizo na uwezo, kaya Milioni 1.2 sawa na asilimia 32.3, Serikali imejipanga kuanza ugharimiaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kundi hilo ambalo linatambuliwa kama kaya zenye umasikini uliokithiri zinazotambuliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), unaohusika na Mpango wa kunusuru kaya masikini.
“Kifungu cha 25 cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Sura namba 161 kimeanzisha Mfuko wa kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo, ambapo Serikali imejipanga kuanza ugharamiaji wa Bima ya Afya kwa wote kwa kaya Milioni 1.2 ambazo zinatambuliwa kama kaya zenye umaskini uliokithiri,” amesema Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kushirikisha wadau mbalimbali ikijumuisha watoa huduma za afya na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote unatekelezeka kwa ufanisi mkubwa, hivyo wananchi ambao hawana uwezo watanufaika na huduma hizo.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Wizara inaendelea kuimarisha ubora wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma kwa kuboresha miundombinu, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, uendelezaji wa wataalamu wa ubingwa na ubingwa bobezi, uanzishwaji wa kada mpya za tiba pamoja na kuimarisha huduma za uzazi wa dharura na watoto wachanga (CEMONC) katika ngazi ya msingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt. Irene Isaka amesema NHIF imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama kwa kusimamia utekelezaji wa miongozo mbalimbali ya tiba ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mtindo bora wa maisha kwa lengo la kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Isaka amesema mfuko huo unaendelea kutumia mbinu mbalimbali za utoaji wa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa wote kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama vile Televisheni, Redio pamoja na mitandao ya kijamii.
“Kufuatia wananchi kujiunga wakati tayari ni wagonjwa inasababisha uwepo kwa matumizi ya huduma yasiyo na uwiano na michango inayokusanywa, hivyo mfuko kuwa na matumizi makubwa kuliko michango, kuanzishwa kwa sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kunalenga kupunguza changamoto hii,” amesema Dkt. Irene.