Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Thobias Makoba, amesema kuwa Idara ya Habari (Maelezo) Tanzania Bara na Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar zimedhamiria kuimarisha ushirikiano ili kuongeza ufanisi wa mawasiliano kati ya Serikali na wananchi wa pande zote za Muungano.
Makoba ameeleza dhamira hiyo Oktoba 25, 2024 mjini Unguja, Zanzibar baadaa ya kufanya ziara katika ofisi za Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar na kukutana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bi. Asha Juma Khamis.
“Idara hizi mbili zina majukumu muhimu sana katika kuratibu mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, hivyo ni muhimu kuimarisha ushirikiano wa ofisi hizi ili kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi katika usimamizi wa sekta ya habari nchini na katika kuratibu mawasiliano kati ya Serikali na wananchi”, ameeleza Msemaji Mkuu wa Serikali.
Amesema ushirkiano huo utagusa maeneo mbalimbali yakiwemo kubadilishana taarifa, kujenga uwezo wa watumishi pamoja na mafunzo hususani katika teknolojia zinazoibukia na njia za kisasa za upashaji habari ili kuzifanya idara hizo kufanya kazi kwa weledi hasa katika kipindi ambacho dunia imekuwa na upotoshaji wa taarifa kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano.
Aidha, Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Thobias Makoba pamoja na mwenyeji wake, Kaimu Mkurugenzi wa Maelezo Zanzibar, wametumia fursa hiyo kujadili maandalizi ya Kikao Kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kinachotarajia kufanyika mwezi Macchi 2025.
Kwa upande wake, Bi. Asha Juma Khamis ameelezwa kufurahishwa na ziara hiyo kwa sababu ushirikiano wa Idara hizo ni kielelezo tosha cha namna Idara hizo zinavyotekeleza majukumu yake kwa manufaa ya Serikali zote na wananchi kwa ujumla.
“Sisi kwetu ni faraja kubwa kutembelewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw, Makoba, kwani ni mara yake ya kwanza kututembelea tangu ateuliwe mwezi Juni mwaka huu na ni imetupa hamasa na ari mpya ya kuimarisha ushirikiano wetu”, ameeleza Asha.
Idara hizi zimekuwa na utamaduni wa kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya usimamizi wa sekta na kuzisemea Serikali katika utekelezaji wa Sera, mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo, na pia kufanya ziara za kubadilishana uzoefu, mafunzo pamoja na kushiriki Vikao Kazi mbalimbali vinavyoandaliwa na Idara hizo.