Home LOCAL FCS NA LATRA CCC WASAINI MAKUBALIANO MRADI WA KULINDA NA KUTETEA HAKI...

FCS NA LATRA CCC WASAINI MAKUBALIANO MRADI WA KULINDA NA KUTETEA HAKI ZA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA USAFIRI WA ARDHINI 

Na Neema Mathayo, Dar-es-Salaam

Asasi ya Foundation for Civil Society (FCS) na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za  Usafiri Ardhini (LATRA CCC) leo tarehe 22 Oktoba 2024 wamesaini makubaliano (MoU) ili kuimarisha ulinzi wa walaji na haki zao ndani ya sekta ya usafiri ili kuwepo na huduma bora kwa wasafirishaji na wasafiri.

Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge amesema kuungana kwa FCS na LATRA CCC ni muunganiko unaokwenda kutengeneza mazingira bora ya walaji katika sekta ya usafiri wa ardhi, kukuza ubora wa kibiashara na kuhamasisha ukuaji wa biashara.


Amesema ushirikiano huo ambao umelenga kuwakilisha maslahi ya walaji wanaotumia usafiri wa ardhi ulio na udhibiti kwa ajili ya bidhaa na huduma katika nchi ambapo MoU itahakikisha wasafiri na wasafirishaji kwa njia ya ardhini wanapata huduma bora zenye kukidhi matakwa ya kitaifa na kimataifa.
Aidha amesema ushirikiano huo wa kimkakati utahusisha kubuni na kutekeleza mipango inayokuza haki za walaji na kulinda bidhaa na huduma za usafiri wa ardhi zinazodhibitiwa.


“Katika kushirikiana na LATRA CCC, wadau muhimu katika kukuza ulinzi wa walaji katika sekta ya usafiri wa ardhi, FCS itatumia utaalamu wake katika kujenga uwezo kusaidia LATRA CCC katika kutafuta rasilimali muhimu za kutekeleza mipango inayolenga kulinda haki za walaji nchini Tanzania,” amesema Bw.Rutenge.

Amesema kwa miongo miwili iliyopita, FCS imeweka mtazamo wa kuzingatia raia, ikilenga kukuza uwezo wa raia. ahadi yao ya kulinda walaji inatokana na dhana hio.
Kuhusu haki muhimu ambazo walaji wanazo, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata malipo ya haki kwa madai, elimu kuhusu usafiri wa ardhini, na uhakikisho wa ubora kwa kuzingatia changamoto pana ambazo walaji wanakabiliana nazo katika kupata bidhaa na huduma za usafiri zilizo na udhibiti na pia mkataba huo ni miaka mitatu ambayo itakwenda kutatua changamoto mbalimbali na kuimarisha huduma na kuwa bora zaidi.
Ulinzi mzuri wa walaji katika sekta ya usafiri ni wa umuhimu na ushirikiano kati ya wadau wa maendeleo, na ushirikiano huu utaimarisha mifumo ya ulinzi wa walaji na kuhakikisha kuna hatua madhubuti za kulinda walaji, amesema.


Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa LATRA CCC, Daud Daudi amesema kupitia makubaliano hayo ya ubia sasa watatengeneza na kutekeleza miradi mbalimbali hasa katika elimu kwa walaji katika makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, wajawazito, wazee na watumiaji wengine wa huduma za usafiri wa ardhini pamoja na kujiongezea uwezo kiutendaji.

“Tanzania inavyosonga mbele kuelekea kukuza mazingira yanayosaidia juhudi za pamoja za kukuza taratibu za biashara zinazofaa na kuwapa walaji maarifa, FCS na LATRA CCC tunatarajia kutekeleza mpango mpana wa ulinzi na haki za walaji katika sekta ya usafiri nchini Tanzania, tukikuza uwezo wa walaji, kutetea haki zao na kuimarisha ushirikiano na wadau muhimu,” amesema Bw.Daud. 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here