Dar es Salaam, Oktoba 15, 2024. Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, na kampuni ya AMSONS ya Uswisi, wameingia makubaliano ya kuwekeza $320 milioni (zaidi ya Sh800 bilioni) katika upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya na kuanzisha kiwanda kipya cha saruji Tanga.
Hayo yamesemwa leo (Oktoba 15) jijini Dar es Salaam na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Bw. Mchechu alisema kati ya fedha hizo, $190 milioni (yapata Sh513 bilioni) zitatumika kwaajili wa ujenzi wa kiwanda kipya Tanga na $130 milioni (Sh351 bilioni) ni kwaajili ya upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya.
“Hivi ninavyozungumza tayari tumeshafanya maamuzi ya kimsingi. Kazi zilizobakia ni za kimenejimenti, ikiwemo kumalizia mpango wa biashara na hatua nyingine za kifedha,” alisema Bw. Mchechu.
Alisema mradi huu wa upanuzi wa kiwanda cha saruji Mbeya na ujenzi wa kiwanda kipya Tanga, unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili hadi mitatu, utapelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa klinka mara kumi.
Kwa kiwanda cha Mbeya, alifafanua, uzalishaji wa klinka, malighafi muhimu kwa utengenezaji wa saruji, unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 1,000 kwa siku hadi kufikia tani 5,000.
Aliendelea kufafanua kuwa kwa upande wa kiwanda kipya cha Tanga, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 5,000 za klinka kwa siku.
“Kuongeza kwa uzalishaji kutatufanya tuendelee kulikamata vizuri soko la nyanda za juu kusini ambalo tumekuwa tukilihudumia kwa Zaidi ya asilimia 70 kwa muda mrefu,” alisema Bw. Mchechu.
Aliongeza: “Uwekezaji huu pia utakuwa mwanzo wa kupenye kwenye nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”
Bw. Mchechu alisema uwekezaji huo ni matokeo ya uboreshwaji wa mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais, Dr. Samia Suluhu Hassan.
“Uwekezaji huu ni sehemu ya mabadiliko ambayo Mhe. Rais amekuwa akitamani kuyaona katika mashirika ambayo Serikali ina hisa,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugezi wa fedha wa AMSONS Bw. Ahmed Mhada alisema kukamilika kwa mradi wa upanuzi na ujenzi wa kiwanda kipya kutapelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kutoka tani milioni 1.1 kwa mwaka hadi kufikia tani milioni 4.2.
“Inatarajiwa kuongezeka kwa uzalishaji kutapelekea kuongezeka kwa gawio mara 10 ya lile ambalo Serikali ilipata mwaka jana,” alisema Bw. Mhada.
Serikali, ambayo inamiliki asilimia 25 ya hisa, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, mwaka jana ilipata gawio la Sh3 bilioni, ikiwa ni miaka 10 ipite bila kampuni hiyo kutoa gawio.
Kama ongezeko la uzalishaji linatarajiwa kuongeza gawio mara 10, tafsiri yake ni kuwa serikali inatarajia kuanza kupata Sh30 milioni kama gawio baada ya mradi kukamilika.
Kwa upande wa ajira, Bw. Mhada, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo, kutazalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 12,000.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kiwanda cha Saruji Mbeya, Prof. Siasa Mzenzi, alimshukuru Mhe. Rais kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji nchini.
“Anachofanya Mhe. Rais, kinavutia wawekezaji kuwekeza nchini. Tuko tayari kusimamia uwekezaji huu ipasavyo kwa maslahi mapana ya Taifa letu na watu wake,” alisema Prof. Mzenzi.
Kadri siku zinavyozidi kwenda, idadi ya watu inazidi kuongezeka, na hatimaye mahitaji ya saruji yanazidi kupaa.
Mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka jana, uzalishaji wa saruji Tanzania ulikuwa tani milioni 11 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 7.5.
Kiwanda cha Saruji cha Mbeya kinamilikiwa kwa ubia kati Kampuni ya Amsons kutoka Holcim ya Uswisi (65%), Serikali ya Tanzania kupitia kwa Msajili wa Hazina (25%) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wenye hisa (10%).