Home LOCAL DKT SLAA AIPASUA CHADEMA, HAWAKUJIANDA WANAJIFICHA KWENYE MALALAMIKO.

DKT SLAA AIPASUA CHADEMA, HAWAKUJIANDA WANAJIFICHA KWENYE MALALAMIKO.

Kada na kiongozi muandamizi wa zamani wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, ameshutumu vikali chama hicho kwa kushindwa kujiandaa kikamilifu kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji, na vijiji.

Katika kauli yake isiyo na kificho, Slaa amewapa somo Chadema, akiwataka wafahamu kwamba kwenda kulalamika kwa mataifa ya Magharibi kuhusu mchakato na matokeo ya uchaguzi kutawafanya wajiulize maswali magumu kuhusu maandalizi yao hafifu.

Slaa pia amemkosoa vikali Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, kwa kushindwa kutoa maelekezo ya wazi kwa viongozi wa ngazi za chini na wadau wa chama, jambo ambalo limesababisha kukwama kwa maandalizi ya uchaguzi huo.

Kutokana na hali hii, ni dhahiri kwamba Chadema wanajua wazi kuwa wanakabiliwa na kushindwa vibaya kwenye uchaguzi ujao, na karata pekee waliyobakiwa nayo ni kutoa visingizio vya mchakato wa uchaguzi ili kuficha udhaifu wao mkubwa wa kutokujiandaa ipasavyo.

Katika mazungumzo yake, Dkt. Slaa alitilia mkazo umuhimu wa chama kuwa na mikakati ya kuwajengea uwezo wananchi, akieleza kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Tanzania hawajawahi kupewa mwongozo madhubuti wa kujitegemea katika harakati za kisiasa.

“Usitegemee wananchi wawe mstari wa mbele, wanahitaji kuongozwa… CHADEMA mliwajengea uwezo? Upi? Kama mliwajengea uwezo wamefika wakashindwa kutekeleza, wananchi wajibu wao nini?” alihoji Dkt. Slaa, akisisitiza kuwa ni jukumu la viongozi wa kisiasa kuwaongoza wananchi na kuwapa moyo wa kusimama kidete kwa ajili ya haki zao.

Dkt. Slaa alitoa mfano wa matukio mbalimbali ya siku za karibuni likiwamo tukio la Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) kuchoma vitenge vilivyokuwa vimetolewa kama zawadi na Rais Samia Suluhu Hassan. Tukio kama hilo ni ishara ya namna chama kimeshindwa kuleta ushawishi wa kutosha kwa wananchi.

“Kwenye suala hili kwa mfano la kuchoma kanga na vitenge, wananchi hawakumualika Rais Samia, nyinyi ndiyo viongozi mliomualika, mlikwenda kama chama kwenda kumbana Samia kwamba ulitupa zawadi, sasa leo tunataka kuchoma hizi zawadi na mkachoma mbele yake? Wananchi mtawaingiza kwenye matatizo tu bila sababu”, amesema Dkt. Slaa na kuongeza,

“Wananchi wana jukumu lao, wananchi mliwaomba kwenye maandamano wametokea. Wananchi wanahitaji kupewa ujasiri, na kauli za vyama vya upinzani juu ya maandamano zilitokaje?”

Aidha Dkt. Slaa amezungumzia suala la maridhiano akilitaja kuwa halikuwa shirikishi kwani CHADEMA walikaa kwenye meza moja na serikali katika mchakato wa maridhiano bila kuwa wazi kwa wananchi. Alidai kuwa kitendo cha viongozi wa chama kukaa na serikali kimya kimya kiliwafanya wananchi kuendelea kukosa ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika harakati za kisiasa.

“Leo unategemeaje wananchi walipuke wakati nyinyi wenyewe mlikuwa mnakaa meza moja na serikali mkinywa juisi… Vitendo vile vilifanya wananchi waendelee kulala,” alisema Dkt. Slaa, akiongeza kuwa chama kilipaswa kuwa na mikakati ya wazi na madhubuti ya kushirikiana na wananchi ili kuongeza hamasa katika kudai haki.

Pia, Dkt. Slaa alieleza kuwa chama kinachotaka kushinda na kuongoza lazima kiwe na mbinu nyingi na za kisasa za kufanikisha malengo yake. Alihoji kama CHADEMA imewahi kuwa na mbinu zaidi ya elfu moja kama ambavyo chama tawala, CCM, hujigamba kuwa nacho.

“CCM wana mbinu elfu moja, nyinyi CHADEMA mna ngapi? Mliwahi kutoka hadharani kutuambia?” alihoji Dkt. Slaa,

Ni ishara nyingine kwamba Chadema, badala ya kutengeneza mipango ya kushindana kidemokrasia, wanaendelea kujificha nyuma ya kelele za malalamiko na hoja zisizo na msingi, huku wakiwaacha wanachama na wafuasi wao katika mkanganyiko na kukata tamaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here