Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuweka utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi wake ikiwemo kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa kada zote ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Agizo hilo amelitoa leo Oktoba 10, 2024 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Wakala huo mkoani Tabora ambapo amesisitiza Wakala huo kuandaa mpango wa mafunzo wa mwaka mzima kwa watumishi wote ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
“Ni muhimu kutoa fursa za mafunzo kwa watumishi waliopo chini yako, teknolojia inabadilika katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, hivyo ili kuwa na wataalam wazuri ni lazima kuendana na mabadiliko ya teknolojia mpya”, amesema Dkt. Msonde.
Aidha, Dkt. Msonde ametoa rai kwa watumishi wa Wakala huo kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia kanuni, miongozo, sheria na miiko ya taaluma zao ili kuboresha utendaji wa Wakala huo.
Amesisitiza ushirikiano kati ya Viongozi wa Wakala huo na watumishi pamoja na kusisitiza uwazi na uwajibikaji baina yao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi, Mohamed Besta amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa ataendelea kujenga weledi na kuwapatia ujuzi watumishi wa Wakala huo nchini kote ili kujenga taswira nzuri ya taasisi hiyo katika utoaji wa huduma bora.
“Nikuhakikishie Naibu Katibu Mkuu, nitaendelea kuwajengea uwezo watumishi waliopo chini yangu, pia kukijengea uwezo kitengo chetu cha TECU ili kuendelea kusimamia vizuri miradi yetu.
Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Tabora, Mhandisi, Raphael Mlimaji amesema mkoa wa Tabora una mtandao wa barabara zenye urefu wa KM 2,188, kati ya hizo 827.23 ni za lami na 1,360.86 ni za changarawe.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.