Akiwa katika banda hilo, Mhe. Biteko alipokea maelezo kutoka kwa Bi. Lulu Mengele, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, aliyewasilisha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba. Bi. Mengele alielezea jinsi Mfuko wa NSSF unavyowahudumia wachimbaji madini, ambao wengi wao ni wanachama wa Mfuko huo, na jinsi wanavyonufaika na huduma za kidijitali kupitia mfumo wa NSSF Portal.
Mfumo huu wa kisasa unawawezesha wanachama, waajiri, na wadau kufikia huduma mbalimbali, ikiwemo kuwasilisha michango, kupata taarifa za mchango, kufuatilia salio, na kufungua madai ya mafao kwa urahisi popote walipo. Bi. Mengele alisisitiza kuwa hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa ufanisi zaidi kupitia mifumo ya kidijitali.
Maonesho hayo ya Teknolojia ya Madini yamezinduliwa rasmi na Mhe. Dotto Biteko na yanaendelea hadi tarehe 13 Oktoba 2024, yakilenga kukuza uelewa wa teknolojia bora katika sekta ya madini.