Home LOCAL BRELA KUKUTANA NA WADAU WAKE WA SEKTA ZA UMMA NA SEKTA BINAFSI 

BRELA KUKUTANA NA WADAU WAKE WA SEKTA ZA UMMA NA SEKTA BINAFSI 

WAKALA wa Usajili wa Biashaa na Leseni (BRELA), Oktoba 25 mwaka huu, wanatarajia kukutana na wadau wake kutoka sekta ya umma na sekta binafsi kwa lengo la kujadili fursa, mafanikio na changamoto za biashara kwa ujumla.

 Katika taarifa iliyotolewa leo Oktoba 23, mwaka huu na Kitengo cha Mawasiliano cha BRELA, imesema kwamba mkutano huo ni wapi pili kufanyika utawakutanisha washiriki wapatao 300 kutoka taasisi mbalimbali nchini na dhumuni likiwa ni kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hiyo na wadau wake.

Pia imesema kwamba dhumuni lingine ni kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA na taasizi zingine zinazoratibu urasimishaji wa biashara nchini huku Kauli mbiu ya mkutano huo ni , “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation).

 Kaulimbiu hiyo, inakwenda sambamba na maagizo na maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo inasomana ifikapo Desemba mwaka huu, Pia taarifa hiyo imesema kwa kuwa urasimishaji wa biashara ni mchakato ni vema kupitia mkutano huo sekta za umma zinazoratibu urasimishaji wa biashara nchini wakasikiliza namna bora ya sekta binafsi inavyopenda ihudumiwe kupitia mifumo kusomana.

Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari nchini, imesema kwamba kutokana na uzoefu uliopatikana katika mkutano wa kwanza wa wadau wa BRELA uliofanyika Oktoba 27, 2023 na kuhudhuriwa na washiriki wapatao 350, ulitoa mwanga na kuonesha umuhimu wa kukutana na kukaa pamoja na wadau kila mwaka ili kubaini fursa, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo sekta binafsi.

 “Mikutano kama hii kwa kiasi kikubwa inasaidia kupata uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kupata majawabu ya fursa, mafanikio na changamoto na inatarajiwa katika mkutano wa mwaka huu wadau wataweza kupata mrejesho wa majukumu yanayofanywa na BRELA ikiwemo,  kupata mrejesho wa maoni.

Pia kupata mrejesho kuhusu ushauri na mapendekezo ya wadau kwenye mkutano uliofanyika mwaka jana, kupata mrejesho wa huduma za BRELA na kuweka mkakati wa pamoja ili kuboresha huduma zinazotolewa na kupata maoni juu ya utendaji kazi wa BRELA hasa matumizi ya mifumo kwa kusomana na mifumo ya taasisi zingine.

Aidha mkutano huo utajadili mada kuhusu mifumo ya taasisi za Serikali kusoma na uwezeshaji kibishara nchini na kubaini changamoto zinazowakabili wadau na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Pia utakuza uelewa wa wadau kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utoaji wa huduma za usajili, ulinzi na utoaji leseni ili kuimarisha utekelezaji wa sheria za nchi na  Kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya sekta ya biashara nchini ikiwemo fursa zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia na namna yanavyochochea ukuaji wa biashara.

Mkutano huo wa Pili wa BRELA na Wadau wake utawakutanisha wadau zaidi ya 300, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za umma, sekta binafsi, taasisi miamvuli, wafanyabiashara, wanazuoni, wajasiriamali na mawakili kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Aidha utakuwa sehemu ya kubadilishana uzoefu utakaowezesha  kuboresha na kuimarisha huduma pamoja na kuongeza ufanisi na tija kwenye utoaji wa huduma na utasaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo wateja na wadau wa BRELA.

Taarifa hiyo imesema mkutano huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, utaendeshwa kwa muundo wa mdahalo ambao utawezesha watoa mada, wachagizaji na waongoza mijadala kuhusiana na mada zilizopo kuibua mjadala kulingana na mada husika.

Washiriki wapatao 300 wanatarajiwa kushiriki katika Mkutano huu ambapo Taasisi mbalimbali zimeonesha nia ya kushiriki katika Mkutano kama washiriki na baadhi wakiwa sehemu ya wadhamini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here