Na; Mwandishi wetu, GEITA
Wito umetolewa kwa Watanzania kutunza sarafu kwa kuwa ni nyara ya serikali na tunu ya taifa ambayo kila mmoja ana wajibu kuhakikisha haiharibiwi.
Akizungumza Oktoba 8, 2024 katika mkutano maalum uliowakutanisha taasisi za fedha, wachimbaji wadogo wa madini, na wajasiriamali mkoani Geita, Meneja Msaidizi wa Mawasiliano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Noves Mosses, amebainisha kuwa kutengeneza pesa kunahitaji gharama kubwa.
“Tunatoa pesa sehemu fulani ili kuzitengeneza, (kuchapisha) hivyo gharama za kutengeneza sarafu na noti ni kubwa sana,” amesema Bi. Mosses.
Aidha, Bi. Mosses ameongeza kuwa Benki Kuu imepata taarifa za imani potofu katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji, ambapo watu huchana noti kwa imani za kishirikina kama njia ya kuepuka ‘Chuma Ulete’.
Alisisitiza kuwa “tabia hii ni uharibifu wa fedha, na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya kosa hilo kwa mujibu wa sheria. Kuna kifungo, faini, au vyote kwa pamoja kwa kosa hilo“
Miezi michache iliyopita nilikuwa Mwanza, na mlikuwa mashuhuda wa watu waliokuwa wanarusha pesa chini kwenye sherehe.
Hii ni moja ya elimu tunayoitoa mara kwa mara kupitia Benki Kuu, ikiwataka watu kutumia vikapu maalum kwa ajili ya kutunza pesa,” amefafanua Bi. Mosses.
Kwa upande wake, Afisa Mkaguzi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Mamy Katikiro, amesema Benki Kuu inatambua changamoto zinazotokana na taasisi ndogo za fedha ambazo hazijasajiliwa, hasa zile zinazotoa mikopo mitandaoni.
Alisema wamepokea malalamiko hayo tangu mwaka jana.
“Kumekuwa na wimbi la taasisi zinazotoa mikopo mitandaoni ambazo hazijasajiliwa, na Benki Kuu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa taasisi hizo kusajiliwa na BoT,” amesema Bi. Katikiro.
Amesisitiza kuwa BoT imeanzisha kampeni ya “ZINDUKA USIUMIZWE” ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mikopo hiyo, ambayo imekuwa ikipewa majina kama “Kausha Damu” kutokana na masharti magumu yanayowaumiza wananchi.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kusoma mikataba ya mikopo kabla ya kukopa ili kuelewa masharti na wajibu wao wakati wa kurejesha fedha hizo.
Mkutano huo umefanyika kwenye maonesho ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita yanaondelea mpaka tarehe 13 Oktoba, 2024.