Home BUSINESS BoT: WANAWAKE WACHIMBAJI TUMIENI FUSHA ZILIZOPO KWENYE TAASISI ZA FEDHA

BoT: WANAWAKE WACHIMBAJI TUMIENI FUSHA ZILIZOPO KWENYE TAASISI ZA FEDHA

 

Meneja Msaidizi wa Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Noves Mosses, akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wachimabaji wadogo wa Madini, Wamachinga na Wajasiriamali na taasisi za fedha katika maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita. 

Joshua Manga Mchambuzi masula ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT akizungumza katika mkutano huo. 

Na; Mwandishi wetu, GEITA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wanawake wachimbaji wa madini kutumia kila fursa inayotolewa na Benki hiyo pamoja na taasisi nyingine za kifedha ili kuboresha shughuli zao za uchimbaji na kujenga mitaji.

Akizungumza wakati wa akifungua mkutano maalum uliowakutanisha taasisi za fedha, wachimbaji wadogo wa madini, na wajasiriamali wakiwemo machinga, katika viwanja vya EPZ Bombambili, Geita, Meneja Msaidizi wa Mawasiliano BoT, Bi. Noves Mosses, alisisitiza kuwa mafanikio ya wachimbaji wadogo wa madini yanahitaji juhudi kubwa na mipango madhubuti katika kujitafutia mitaji ya kuendeleza shughuli zao

Bi. Mosses amesema kuwa BoT imeanzisha utaratibu wa kununua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji wadogo kwa bei nzuri inayolingana na soko la dunia. Hii inalenga kuwapa wachimbaji nafasi ya kuuza dhahabu zao kwa faida zaidi na kwa urahisi mkubwa.

“Pia, Benki Kuu imepunguza gharama za uchenjuaji wa dhahabu ili kuwawezesha wachimbaji kufanya biashara yao kwa urahisi zaidi,” ameongeza.

Aidha, Bi. Mosses amehimiza wanawake wachimbaji kutumia fursa zinazotolewa na benki nyingine ambazo zitaelezwa katika mkutano huo. Alieleza kuwa taasisi za fedha itatoa maelezo kuhusu madirisha na huduma mbalimbali wanazozitoa ambazo zinaweza kusaidia katika kukuza mitaji na kuboresha biashara za uchimbaji wa madini.

“Naamini mkipata uelewa wa kina kuhusu fursa hizi, mtaweza kuimarisha biashara na mitaji yenu na kuendelea kusonga mbele katika shughuli za uchimbaji wa madini,” amesema Bi. Mosses.

Kwa upande wake Joshua Mganga, Mchambuzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amewaeleza kwa undani wachimabaji hao umuhimu wa mpango wa BoT wa kununua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji wadogo.

Amebainisha kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata bei nzuri wanapouza dhahabu yao BoT kulingana na bei ya soko la dunia, huku wakifaidika na malipo ya haraka, ambayo hufanyika ndani ya saa 24.

Mganga amesisitiza kuwa ununuzi wa dhahabu na BoT siyo tu una faida kwa wachimbaji, bali pia unachangia kukuza uchumi wa nchi kwa kuongeza akiba ya dhahabu, ambayo inasaidia kuimarisha thamani ya shilingi. Hii inapunguza utegemezi wa fedha za kigeni na kuweka msingi mzuri wa kifedha kwa taifa.

Amefafanua zaidi kuwa dhahabu ni rasilimali muhimu kwa uchumi wa Tanzania, na kwa BoT kununua dhahabu hiyo, inawezesha kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uthabiti wa sarafu ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine za kigeni.

Pia ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kuwa BoT inatoa bei ya kila siku inayolingana na soko la dunia, wachimbaji wanapata uhakika wa bei nzuri bila kupitia changamoto za kuuza dhahabu nje ya nchi, ambako wanaweza kukumbana na ada na ucheleweshaji wa malipo.

Mganga amewahimiza wachimbaji wadogo na wa kati kuitumia fursa hii kikamilifu ili kuleta faida kubwa kwao na kwa uchumi wa nchi.

   

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here