Home BUSINESS BASHE: ACHENI SERIKALI IJENGE MFUMO IMARA WA TUMBAKU NCHINI

BASHE: ACHENI SERIKALI IJENGE MFUMO IMARA WA TUMBAKU NCHINI

Serikali yatuma salamu kwa wafanyabiashara na viongozi wababaishaji wanaokandamiza wakulima wa Tumbaku kwa kuchelewesha malipo ya fedha za ruzuku ya mbolea ili kuacha mara moja tabia hiyo laa sivyo watatajwa hadharani.

Salamu hizo zimetolewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) tarehe 9 Oktoba 2024 kwenye mkutano wa hadhara wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kwenye ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.

“Toka mwezi wa tano nimeagiza vyama vikuu vya ushirika kulipa fedha za ruzuku kwa wakulima, na nimezuia shilingi bilioni 13 fedha za Umma kwa ajili ya wakulima nikiwa kama Waziri mwenye dhamana na siyo ruzuku ya Chama cha Ushirika. Nataka niletewe mkeka wenye jina la mkulima, Chama chake cha Msingi, Chama chake Kikuu cha Ushirika, mifuko ya NPK aliyotumia na akaunti namba yake ili fedha ilipwe moja kwa moja kwa mkulima,” amesema Waziri Bashe.

Ameongeza kuwa fedha zikilipwa Chama cha Ushirika zitapangiwa matumizi mengine badala ya kumlipa mkulima.

Aidha, amesikitishwa na kitendo cha Meneja wa Chama cha Ushirika cha WETCO cha kupotosha kuhusu malipo ya ruzuku kwa wakulima, huku ukweli ni fedha zipo kwa ajili ya malipo kwa wakulima ambao wamepokea mbolea tangu Septemba 2024. Ameongeza kuwa ikiwezekana WETCO atafutiwa leseni pamoja na wafanyabiashara wengine wababaishaji kama wakulima hawalipwi kwa wakati.

“Serikali imepambana sana kuinua tasnia ya Tumbaku ambayo ilikufa Tabora kutokana na wanasiasa na Ushirika mbovu. Kuna nchi kama Malawi, Zambia, Zimbabwe na Mozambique ambazo hawana Vyama vya Ushirika bali mfumo wa Serikali, mkulima na mnunuzi yote katika kuondosha mzunguko wa malipo kupitia Ushirika,” amesema Waziri Bashe.

Naye Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amesisitiza maelekezo ya Waziri Bashe na kusema “ni maelekezo ya msingi ambayo yeye na Mhe. Rais Dkt. Samia wanakubaliana nayo. Hiyo michezo inayofanywa na wafanyabiashara na viongozi acheni na badilikeni, sitakuwa tayari kuikubali. Waziri Bashe usihofu kuwataja wanaowahujumu wakulima na ikibidi futa makampuni ambayo hayalipi wakulima kwa wakati.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here