Home BUSINESS BANKI YA CRDB YATUNUKIWA TUZO ZA ‘BENKI BORA’ NA SALAMA TANZANIA...

BANKI YA CRDB YATUNUKIWA TUZO ZA ‘BENKI BORA’ NA SALAMA TANZANIA NA JARIDA LA GROBAL FINANCE

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto), akipokea tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ kutoka kwa Joseph Giarraputo, Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Global Finance, katika hafla iliyofanyika Washington D.C. tarehe 26 Oktoba 2024. Katika hafla hii, iliyofanyika sambamba na Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Benki ya CRDB pia ilitunukiwa tuzo ya ‘Benki Salama.
 
Na Mwandishi Wetu.
 
Washington D.C., 26 Oktoba 2024 – Benki ya CRDB imetambuliwa kwa mara nyingine kama kinara katika sekta ya benki Tanzania kwa kushinda Tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ na ‘Benki Salama Tanzania’ zilizotolewa na Jarida la Global Finance kwenye hafla ya 31 ya Mwaka ya Tuzo za Benki Bora.
 
Tuzo hizo zimetolewa katika hafla iliyofanyika sambamba na Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia huko Washington, D.C. Hii ni mara ya tano mfululizo kwa Benki ya CRDB kushinda tuzo ya Benki Bora Tanzania na mara ya pili mfululizo kwa Benki Salama Tanzania – ikidhihirisha uimara wa Benki hii katika sekta ya fedha.
 
Mafanikio haya yanadhihirisha mkakati wa Benki ya CRDB wa kukua kwa njia endelevu inayowanufaisha wateja, wawekezaji, na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
 
Aidha, tuzo hizi ni kielelezo cha uongozi thabiti wa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Group, Abdulmajid Nsekela, na zinadhihirisha mchango wa Benki ya CRDB katika kuimarisha sekta ya fedha nchini Tanzania na ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati.
 
Tunajivunia sana kwa kutambuliwa kwa mara nyengine kama Benki Bora Tanzania na Benki Salama katika tuzo za Global Finance,” alisema Nsekela. “Tuzo hizi ni ishara kwamba tupo kwenye njia sahihi ya ukuaji – kutoa huduma za kipekee kwa wateja wetu, thamani kwa wanahisa wetu, na kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya fedha nchini.”
 
Benki ya CRDB imekuwa na mwaka wa mafanikio makubwa kutokana na maboresho ya miundombinu ya kidijitali, ambayo imeongeza ufanisi na ubunifu katika utoaji wa huduma. Nsekela alisisitiza kuwa ukuaji wa Benki umetokana na mikakati madhubuti, hali ambayo imeifanya Benki hiyo kuwa chaguo la kwanza kwa Watanzania.
 
“Tuzo hizi hazionyeshi tu dhamira yetu ya kuwa Benki kinara katika utoaji wa huduma bora na zinazokidhi mahitaji halisi ya wateja – bali pia zinaonyesha namna gani tumekuwa tukisikiliza na kufanyika kazi maoni ya wateja na washirika wetu, na jinsi ambavyo wafanyakazi wanajitoa katika kutoa huduma bora,” aliongeza. “Ni heshima kubwa kuwa Benki Salama na Benki Bora Tanzania, tuzo hizi zinatupa nguvu ya kusonga mbele katika kuwawezesha Watanzania na kuimarisha nafasi yetu kimataifa.”
 
Ikiwa na rasilimali za zaidi ya Shilingi trilioni 14, Benki ya CRDB inashikilia nafasi kama benki kubwa zaidi Tanzania, inayotambulika kwa mafanikio endelevu katika viashiria vyotevya kiutendaji vya biashara.
 
Joseph Giarraputo, Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Global Finance, amesema tuzo hizo pia zinatambua jitihada za Benki ya CRDB katika kukuza ujumuishi wa kifedha na kujenga imani ya wateja na wawekezaji akisema, “Katika mwaka uliopita, Benki ya CRDB imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma bora na kujenga imani miongoni mwa wateja na wawekezaji ndani na nje ya nchi.”
 
Wakati wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Washington D.C., Nsekela alishiriki pia kwenye mjadala maalum kuhusu mifumo ya malipo kidijitali ambapo alisisitiza dhamira ya Benki ya CRDB katika kukuza suluhisho za kidijitali zinazoboresha upatikanaji wa huduma za kifedha.
 
Aidha, Nsekela alishiriki vikao vya kimkakati na taasisi za kimataifa kama vile Benki ya Dunia, Exim Bank ya Marekani, MUFG, Yaatra Ventures, na TIAA Mfuko wa Pensheni wa Marekani unaolenga uwekezaji wa kimkakati barani Afrika, akilenga kufungua njia mpya za mitaji na kuiweka Tanzania kama kiungo muhimu kwenye uchumi wa dunia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here