Na Mwandishi, Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara Leseni (BRELA) kuwa wawezeshaji wa Wafanyabiashara kwa kuwasaidia katika kufanikisha kurasimisha biashara zao na siyo kuwa kikwazo.
Maelekezo hayo yametolewa leo Septemba 9, 2024 katika ziara aliyoifanya ofisi za BRELA jijini Dar es Salaamili kujionea utendaji kazi na kujifunza namna Wakala inavyotoa huduma za Sajili mbalimbali. Amewataka wabunifu wote nchini kulinda bunifu zao kwa kuzisajili kisheria ili zisichukuliwe na watu wengine na kujinufaisha nazo bila kufuata utaratibu wa kisheria.

“Ninatoa wito kwa Watanzania wabunifu wote kusajili bunifu zenu kupitia BRELA maana taasisi hii inakazi ya kulinda haki za ubunifu ili kuwawezesha kufaidika na jitihada za ubunifu na hatimaye kuongeza kipato kwa wabunifu na taifa kwa ujumla” amesisitiza Dkt. Jafo.

Aidha, amewataka kutumia kanuni na sheria kusaidia biashara kwenda mbele na sheria ambazo zinakwamisha ziwasilishwe ili ziweze kufanyiwa maboresho kwamba nimuhimu kuelewa jukumu la BRELA ni kujenga misingi na mazingira mazuri ya biashara.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, Prof. Neema Mori, amesema kuwa BRELA imedhamiria kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini yanakuwa bora zaidi kwa kuwawezesha, kuwarahisishia na kutoa usaidizi wa karibu kwa wafanyabiashara wanapo rasimisha biashara, kutoa elimu pamoja na kuwahusisha wadau mbalimbali ili wajue namna.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw.Godfrey Nyaisa amesema kuwa kwa sasa sera ya miliki ubunifu inaelekea kupitishwa na baadae kuwa na sheria ambayo itasaidia ongezeko kubwa la maombi ya ulinzi wa bunifu hizo ambapo kuna jitihada ambazo BRELA inaendelea nazo katika kuhakikisha elimu ya miliki bunifu inafahamika kuanzia ngazi ya shule ya za msingi hadi vyuo vikuu.
Mbali na jukumu la kusajili miliki ubunifu na utoaji wa hataza amesema kuwa BRELA inatoa ufadhili wa Shahada ya Uzamili ya Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaamkwa watu watano kila mwaka ambapo elimu hii mtu atakayoipata itasaidia katika ukuaji wa sekta ya miliki ubunifu nchini.