Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, akizungumza katika kikao kazi cha Wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Septemba 2,2024 Jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Afisa Habari Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akizungumza alipokuwa akiwakaribisha na kutoa neno la utangulizi katika kikao kazi hicho.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Catherine Sungura, akizungumza alipokuwa akiwashukuru Wahariri na waandishi waliojitokeza katika kikao kazi hicho.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM
Katika kuhakikisha changamoto zinazoukabili mtandao wa Barabara zinatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi wa kina, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeweka vipaumbele muhimu vinne ili kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa Barabara zote nchini.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo, ni pamoja na matengenezo ya miundombinu ya Barabara ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika katika maeneneo mbalimbali nchini.
kipaumbele kingine ni kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa Barabara za wilaya ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mvua.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff alipokuwa akitoa wasilisho katika kikao kazi cha Wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Septemba 2,2024 Jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Mhandisi Seff amesema TARURA inaendelea na matengenezo hata pale Barabara na madaraja yanapokamilika ili miundombinu hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.
Aidha, ameeleza kuwa katika kutekeleza majkumu yao wanatumia teknolojia mbadala pamoja na malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya Barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazinga, sambamba na kuzipandisha hadhi Barabara kutoka udongo kuwa changarawe, kutoka changarawe au udongo na kuwa Barabara za lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii.
“Serikali imedhamiria kuboresha na kujenga Barabara nyingi za wilaya ili kurahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi, kwani mpaka sasa tumefanikiwa kuongeza mtandao wa Barabara za wilaya kutoka kilomita 108,946.19 hadi kilomita 144,429.77.
“Hadi kufikia Juni, 2024 Barabara za lami za wilaya zilikuwa kilomita 3,337.66 sawa na asilimia 2.31, kati ya hizo, kilomita 2,743.81 zipo katika hali nzuri, kilomita 445.18 zipo katika hali ya wastani na kilomita 148.68 zipo katia hali mbaya“ ameeleza Mhandisi Seiff.
Katika hatua nyingine Mhanisi Seiff amezungumzia kuhusu ujenzi wa Daraja na uendelezaji wa mto msimbazi, nakwamba eneo la chini la mto huo linatarajiwa kuongezwa kina na kupanuliwa ili kuruhusu maji kwenda Baraharini kwa kasi inayotakiwa.
Amesema mradi huo umeanza rasmi tarehe 16 Februari 2023 ambao unatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (Dola za Marekani milioni 200), Serikali ya Hispania (Euro milioni 30) na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi (Euro 30).
“Hadi sasa asilimia 98 ya watu ambao wanaathirika na mafuriko wamelipwa fidia na wameondoka, lakini pia zipo kaya takribani 314 ambazo zimetambuliwa kuwa zitaathirika na ujenzi na mchakato wa kuandaa daftari la fidia unaanza mwezi Septemba mwaka huu“ amesema.