Home LOCAL TANROADS YADHAMIRIA KUBORESHA MIUNDOMBINU NCHINI

TANROADS YADHAMIRIA KUBORESHA MIUNDOMBINU NCHINI

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Ephatar Mlavi akizungumza wakati wa mkutano na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika leo Septemba 26, 2024 Jijini Dar es Salaam. chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina

Kaimu Mkuu wa kitengo cha  Mwasiliano Serikalini Wakala wa Barabara TANROADS  Bi. Aisha Malima akizungumza katika kikao hicho.

Afisa Habari Ofisi ya Majili wa Hazina Bw. Alex Malanga akifafanua akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi katika kikao kazi hicho.

Na;Mwandishi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imedhamiria kuhakikisha inaboresha miundombinu ya Barabara kwakutenga zaidi ya shilingi Bilioni 900 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Barabara iliyoharibiwa kutokana na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.

Hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha miundombinu muhimu ya usafirishaji inabaki imara na inahudumia wananchi kwa ufanisi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Ephatar Mlavi, wakati wa mkutano na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambao uliratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkutano huo ulilenga kuelezea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kwenye sekta ya ujenzi na maendeleo ya miundombinu.

Kwa mujibu wa Mlavi, TANROADS inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa zaidi ya kilometa 37,000 kote nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi, ukarabati, na matengenezo ya barabara na madaraja.

Hii inaongeza ufanisi wa miundombinu ya usafirishaji na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Mbali na shughuli za ukarabati wa barabara, TANROADS pia imepokea fedha kwa ajili ya kusimika taa za barabarani, ambazo zinalenga kuboresha usalama wa barabarani na kupendezesha mandhari ya miji mikubwa nchini

Hatua hii inatarajiwa kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara hasa wakati wa usiku na kupunguza ajali zinazoweza kutokea kutokana na giza.

Kuhusu ujenzi wa daraja la Jangwani, linalounganisha Magomeni Mapipa na Fire, Mlavi ameeleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na mkandarasi, na mkataba huo unatarajiwa kusainiwa mwezi ujao.

Daraja hili ni mojawapo ya miradi ya kimkakati inayolenga kupunguza msongamano wa magari na kuimarisha mawasiliano kati ya maeneo muhimu ya jiji la Dar es Salaam.

Aidha, Mlavi alizungumzia changamoto za wakandarasi wazawa katika kupata kazi kubwa za ujenzi, akisema hali hii inatokana na ukosefu wa mitaji mikubwa.

Hata hivyo, alifafanua kuwa wakandarasi wa ndani wanachangia takriban asilimia 31.60 ya miradi inayosimamiwa na TANROADS, ikiwa ni ishara ya mchango wao katika maendeleo ya miundombinu ya nchi.

Serikali inaendelea kuhamasisha ushiriki wa wakandarasi hawa kwa kuwajengea uwezo wa kifedha na kitaalamu ili waweze kushindana kwenye miradi mikubwa zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here