Home BUSINESS SKIMU ZA UMWAGILIAJI, MBOLEA NA MATREKTA KULETA MATUMAINI KWA WAKULIMA WA NZEGA...

SKIMU ZA UMWAGILIAJI, MBOLEA NA MATREKTA KULETA MATUMAINI KWA WAKULIMA WA NZEGA NA IGUNGA

Ziara ya ukaguzi wa skimu za umwagiliaji na maendeleo ya upembuzi yakinifu wa skimu za umwagiliaji imeendelea leo tarehe 14 Septemba 2024 katika Wilaya za Nzega na Igunga, Mkoani Tabora.

Akikagua eneo linalotarajiwa kujengwa bwawa la maji lenye ukubwa wa hekta 3,205 na ujenzi wa mifereji ya kusafirisha maji, Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo amewahakikishia wanakijiji wa Kata za Choma, Mwasala na Wela na kuwaeleza kuwa Wakuu wa Wilaya zote mbili, Viongozi wa Kijiji, Madiwani na Wataalamu wa Wizara ya Kilimo kwa pamoja watakaa na wakazi wa maeneo hayo ili kutoa elimu na kupokea maoni na changamoto zozote na kubaini endapo skimu hiyo ijengwe na eneo lipi.

Sambamba na hilo, Waziri Bashe amekagua pia skimu ya umwagiliaji ya Mwamapuli na kuielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya tathmini ya kitaalamu kwa lengo la kuongeza kina cha maji na kuongeza na kuboresha mifereji ya maji ili kunufaisha wakulima wa kilimo cha umwagiliaji. “Nimefurahi kukutana na wanakijiji wa eneo la Mwanzugi ambapo ombi lenu la kupatiwa pawatila litafanyiwa kazi; pia Serikali itaweka kitalu cha kuzalisha mbegu bora na kuongeza mbolea za ruzuku.

Akiwasilisha salamu za Wilaya ya Igunga, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Sauda Mtondoo amesema kuwa wananchi wake wanaomba Wizara ya Kilimo isaidie kuongeza Maafisa Ugani, mbegu bora, skimu za umwagiliaji, zana za kilimo na mbolea za ruzuku.

“Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo imefanya jitihada za kuhakikisha kuwa huduma za ugani zinaboreshwa kwa ajili ya kuongeza Maafisa Ugani wa kutosha, kuwapatia vitendea kazi ili kuwa na kilimo chenye tija ili kuondokana na umaskini,” amesema Waziri Bashe.

Ameongeza kuwa Serikali imetoa vishikwambi, pikipiki, soil scanner kwa ajili ya kupima afya ya udongo na programu ya kujenga nyumba za Maafisa Ugani ili waishi vijiini kutoa huduma kwa wakulima. “Tutatenga bajeti maalum kusaidia shughuli za Kilimo kwenye Halmashauri. Na tayari Mikoa 15 na Halmashauri 10 zimepokea magari kwa shughuli za wakulima,” ameongeza Waziri Bashe.

Previous articleWANANCHI WATAKIWA KUTAMBUA NA KUTHAMINI MIRADI YA MAENDELEO
Next articleSEKTA YA UGANI KUPEWA HESHIMA NCHINI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here