Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kuondoa msongamano wa magari makubwa katikati ya Mji wa Songea kwa kujenga barabara ya mchepuo (Songea Bypass) yenye urefu wa kilometa 16 ambapo utekelezaji huo utaenda sambamba na ujenzi barabara ya Songea – Njombe (km 100).
Amesema hayo leo Septemba 24, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Peramiho katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kueleza kueleza kuwa Serikali itasaini Mkataba wa utekelezaji huo ifikapo Mwezi Oktoba, 2024.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni maelekezo yako kufika mwezi ujao Wizara iwe imesaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 16 za kuondoa kero na foleni Songea Mjini pamoja na kilometa 100 za kuelekea Mkoani Njombe”, amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba 2024, Serikali itasaini mkataba wa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Lukuyufusi – Lipapasi – Mkenda (km 60) kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na nchi jirani ya Msumbiji.
“Serikali inakwenda kujenga barabara ya Lukuyufusi – Mkenda barabara ambayo mmeililia kwa muda mrefu na sasa Rais Dkt. Samia anakwenda kuijenga kwa kiwango cha lami”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amebainisha kuwa Wizara ya Ujenzi ipo katika hatua ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Daraja la Mitomoni lenye urefu wa mita 80 litakalounganisha Wilaya ya Songea Vijijini na Wilaya ya Nyasa.