Home LOCAL SERIKALI HAITAPUUZA ASASI ZA KIRAIA-DKT BITEKO

SERIKALI HAITAPUUZA ASASI ZA KIRAIA-DKT BITEKO

Asema Serikali Haina Mpango wa Kusigana Nazo

Aielekeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii Kuratibu Mashirika Kuwa na Malengo Chanya

Yaaswa Kuzingatia Utu na Maadili ya Kitanzania katika Kutekeleza Majukumu yao

Serikali Kuendelea Kushirikiana na Mashirika Kuleta Maendeleo Nchini

Asisitiza Fedha za Wafadhili Zitumike Zilivyokusudiwa

Ayaasa Mashirika Kuwahudumia Watanzania kwa Upendo

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali haitapuuza mchango wa asasi za kiraia kwa kuwa wao ni wadau muhimu na wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kuwaletea Watanzania maendeleo.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 6, 2024 jijini Dodoma wakati akihutubia Mkutano wa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Serikali haitapuuza hata kidogo mchango wenu asasi za kiraia wala kuudogosha kwenye maendeleo ya nchi yetu kwenye nyanja zote ikiwemo za kiuchumi, utawala bora na kijamii kwa sababu ni wadau muhimu, mashirika yote yaliyopo nchini 9,777 yanalenga kuwahudumia Watanzania.’’ Amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kwa kusema kuwa kazi ya Serikali ni kuhudumia Watanzania, ambapo pia kazi ya mashiriki hayo ni kuisaidia Serikali kuweza kutekeleza majukumu yake kwa urahisi na kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi na kuwa hayapaswi kuwa adui wa Serikali bali mshirika na mdau muhimu wa maendeleo.

Ametaja faida zingine za mashirika hayo kuwa ni fedha zilizopatikana ambazo ni shilingi trilioni 2.6 zimezunguka nchi nzima na zaidi ya watu 21,000 wameajiriwa katika sekta hiyo na kuwa yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali hususan katika nyanja za afya, kilimo, elimu, maji na sekta nyingine mtambuka pamoja na kuchangia kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Serikali inategemea kuwahudumia Watanzania katika kila afua mfano afya na hivyo wahudumieni kwa upendo nao watawafurahia na kushirikiana nanyi mahali mlipo,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

Ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara (2020) ambao upo kwenye mapitio, Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020).

Kitabu cha Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa kila mwaka, Mfumo wa Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Digital Mapping Tool – 2023), Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Wizara, Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2022/23 – 2026/27).

‘’Mkakati huo ni uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambao utayawezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupata fedha bila masharti magumu ya ufadhili. Kutokana na umuhimu huo, tarehe 05 Novemba, 2023 wakati wa kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika Jijini Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, alielekeza Wizara kushirikiana na wadau wengine kuanza mchakato wa kuandaa mfuko huo wa ruzuku. Nimejulishwa kuwa tayari mchakato wa uanzishaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund – NBF) umeanza na ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utakuwa shirikishi. Vilevile, nafahamu kuwa Wizara ya Fedha ipo katika mchakato wa uandaaji wa Mwongozo wa Ushirikiano na Asasi Zisizo za Kiserikali ambapo baada ya kukamilika kwa Mwongozo huo, utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hususan katika Bajeti ya Serikali utatambulika na utaongezeka mara dufu.’’ Amesisitiza Dkt. Biteko.

Pamoja na hayo, ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuyasimamia mashirika yasiyo ya kiserikali ili yaweze kuwa mchango chanya kwa jamii, pamoja na kuyaasa mashirika hayo kutumia vizuri fedha wanazozipata kutoka kwa wafadhili kwa kutekeleza kazi zilizokusudiwa huku akiwataka kuzingatia utu na maadili ya Mtanzania katika kutekeleza majukumu yao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameyapongeza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuchagiza maendeleo nchini na kuyaasa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania na kuwa Serikali imejipanga kuweka mikakati ya kuhakikisha ajenda hiyo inafikiwa ili asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ifikapo 2034 na kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ambapo zaidi ya vifo 30000 hutokea kila mwaka.

Naye, Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuiletea nchi maendeleo na Wizara yake itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili mashirika hayo yaendelee kufanya kazi zao nchini.

Naye, Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. Marianne Young amesema kuwa nchi yake itaendelea kushirikikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Bw. Jasper Makala amesema kuwa Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini imeendelea kukua na kuimarika mwaka hadi mwaka sio tu kwa idadi ya Mashirika yaliyosajiliwa, lakini pia kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali.

“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, pamoja na Wizara nyingine za Kisekta na kwamba tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia Sheria, 5 Kanuni na Miongozo ya inayosimamia uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sheria nyingine za Nchi.’’ Amesema Bw. Makala.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here