Home BUSINESS SEKTA YA UGANI KUPEWA HESHIMA NCHINI

SEKTA YA UGANI KUPEWA HESHIMA NCHINI

Maafisa Ugani 23 wa Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora wamepewa moyo na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) na kuelezwa Serikali imewekeza vitendea kazi vya pikipiki, vishikwambi, soil scanners kwa ajili ya upimaji wa afya ya udongo na programu ya kujenga nyumba zao.

Amesema hayo tarehe 14 Septemba 2024 wakati wa ziara yake katika Wilaya za Nzega na Igunga na kuahidi kuwa ataongeza Maafisa Ugani zaidi ya 100 ili wanakijiji wa maeneo hayo waweze kulima mbinu za kisasa na kwa tija zaidi.

“Mkuu wa Wilaya mkitenga eneo kwa ajili ya kitalu cha uzalishaji wa mbegu, Wizara ya Kilimo haitosita kuja kuhakikisha kitalu hicho kinaleta uzalishaji mkubwa wa mbegu katika ukanda wa Wilaya ya Igunga,” amesema Waziri Bashe.

Ameahidi kuwa mabonde ya Wilaya hiyo yatapitiwa na kufanyiwa michoro upya ili kuhakikisha wakulima wananufaika ipasavyo na vizazi vijavyo. “Nawasihi lindeni maeneo ya kilimo na tuwe na mipaka ya maeneo ya Kilimo hususan mabonde ili kulinda rasilimali zinazopitisha njia za maji na zenye uwezo wa kujengewa mifereji ya kupitishia maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,” amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri Bashe amemuelekeza Mkuu wa Wilaya kufanya vikao na wanavijiji kushawishi waanze kujenga maboma ya nyumba ili Wizara ya Kilimo itafute Fedha za kuja kusaidia kumalizia nyumba kwa ajili ya matumizi ya Maafisa Ugani katika kutoa huduma kwa wakulima.

Waziri Bashe pia ameielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutekeleza maeneo yote ya miradi ya umwagiliaji katika Wilaya ya Igunga kwa wakati. Akifafanua zaidi kuhusu takwimu za miradi inayoendelea wilayani humo, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Bw. Raymond Mndolwa amesema kuwa kuna miradi 4 ya mabwawa ambayo ipo kwenye hatua ya usanifu na kuomba kupatiwa ushirikiano wa taarifa za maeneo yanayohusisha ujenzi wa ofisi za kilimo.

Previous articleSKIMU ZA UMWAGILIAJI, MBOLEA NA MATREKTA KULETA MATUMAINI KWA WAKULIMA WA NZEGA NA IGUNGA
Next articleBASHE: SIKIMU YA MZEE SHIJA KUNUFAISHA WAKULIMA WA WILAYA YA KAHAMA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here