Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza juhudi za wakulima wa Mkoa wa Ruvuma katika kuzalisha mazao kwa wingi na kuifanya Tanzania kuwa na usalama na uhakika wa chakula.
Amepongeza wakati aliposimama na kukagua Kituo cha Ununuzi wa Nafaka cha Mbinga Sokoni, Mkoani Ruvuma tarehe 25 Septemba 2024 na kuongea kwenye hadhara ya maelfu ya wananchi waliojitokeza.
Wananchi hao ambao wengi wao ni wakulima, wametakiwa kuepuka bei za walanguzi za mahindi; na kuhakikisha kwa vijijini wasiuze mahindi si chini ya shilingi 500 hadi 600 kwa kilo ambayo ni bei elekezi ya Serikali. Vinginevyo wauze katika vituo vya ununuzi vya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa bei elekezi ya vituo hivyo ya shilingi 700 kwa kilo.
Naye Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amewahakikishia wakulima kuwa ununuzi katika vituo vyote unaendelea; huku Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na sasa ruzuku ya mbegu za mahindi ambavyo vyote vitakuwa na maelekezo ya kufuata kwenye kila mfuko jinsi ya kuhakiki kama ni feki au la.
“Mheshimiwa Rais, wakulima wa Mbinga wanazalisha mazao kadhaa, lakini kwa zao la Kahawa aina ya Arabica wanafanya vizuri kwa mauzo ya Dola za Marekani 5.6 ambayo ni tofauti na kiwango cha wastani wa mauzo nchi nzima kwa Dola za Marekani 4.7,” amesema Waziri Bashe.
Amewahakikishia wakulima kuwa changamoto za Vyama vya Ushirika na mfumo wa kangomba imeanza kufanyiwa kazi ili kuhakikisha mauzo ya wakulima yanaenda kwenye mfumo wa mnada na uwazi katika kuhakikisha mkulima anapokea malipo ndani ya Siku 48.
“Ni marufuku viongozi wa ushirika kukopa fedha kwa majina ya wakulima. Huu ni unyonyaji kwa mkulima,” ameongeza Waziri Bashe.