Na WMJJWM, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu amefungua mafunzo ya siku mbili kuwajengea uwezo Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikari kwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri zote Tanzania bara Septemba 4, 2024 jijini Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) Naibu Katibu Mkuu Felister amesema matarajio ya mafunzo hayo ni kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Maafisa hao kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
“Mashirika yataweza sasa kulipa ada kwa wakati, kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa katika kutekeleza majukumu yao.”Amesema Felister.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Serikali (NaCONGO) Makala Jasper ameishukuru Wizara kwa ushirikiano inaotoa kwa mashirika yote nchini katika ngazi zote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika hayo Mwantumu Mahiza amewataka Wasajili kufanya kazi kwa karibu na NGOs kwenye maeneo yao na kufuatilia shughuli wanazofanya kwa mustakabali wa nchi ya Tanzania.