Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema unahitajika ufadhili unaotabirika, unaoweza kufikiwa, endelevu na wenye uwiano kati ya kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Amesema nchi zinazoendelea zinahitaji zaidi ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikia azma kuzingatia jinsia katika ufadhili huo.
Halikadhalika ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi kufanya mijadala ya kina, kubadilishana uzoefu katika mafanikio, changamoto na mafunzo ili kuweza kupata suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ufadhili unaozingatia jinsia.
Amesema kwa kuunganisha maarifa na utaalamu wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutawezesha kuongeza juhudi za kitaifa na kimataifa na kuharakisha maendeleo katika kufikia malengo ya pamoja ya ufadhili endelevu wa mabadiliko ya tabianchi unaozingatia jinsia.
Makamu wa Rais amesema mkutano huo unapaswa kusaidia katika kuhakikisha ahadi za nchi zilizoendelea za utoaji wa dola milioni 100 kila mwaka zinatimizwa ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya ahadi za nchi hizo za kuwezesha utekelezaji wa mkataba wa Paris.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni kuongeza kasi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ufadhili unaozingatia jinsia. Kutokana na kauli mbiu hiyo, Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuhimiza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabianchi kwenye sera, programu na mikakati katika ngazi zote.
Ametaja sera hizo zinazopewa kipaumbele ni pamoja na usawa wa kijinsia katika kushiriki shughuli za uchumi, kuweka mazigira rafiki kwa wanawake kushiriki katika uongozi na utoaji maamuzi, usawa wa kijinsia katika elimu, matumizi ya teknolojia pamoja na uwezeshaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya mijini na vijijini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Tarehe 02 Septemba 2024.
Makamu wa Rais amesema jitihada hizo za ujumuishi wa jinsia katika masuala mbalimbali zinalenga kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata fursa sawa ya kushiriki, kuchangia na baadae kunufaika na mipango na juhudi za mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kwa kuwa zinafanyika jitihada za kuhakikisha ujumuishaji wa jinsia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hivyo ni muhimu suala la nishati safi ya kupikia kuwa jambo muhimu la kuzingatia katika Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika mjini Baku nchini Azerbaijan.
Amesema Tanzania imebeba nishati safi ya kupikia kama ajenda muhimu ya Taifa ambapo lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia kutoka katika asilimia 7 iliyopo hivi sasa. Ameongeza kwamba jambo hilo muhimu litasaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya nishati asilia ya kupikia ikiwemo mkaa na kuni.
Mkutano huo wa siku tano unahudhuriwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani, wadau wa mazingira, viongozi na watunga sera.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi mara baada ya Ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa kamati hiyo unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Tarehe 02 Septemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Tarehe 02 Septemba 2024.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
02 Septemba 2024
Arusha.