Wakulima wa zao la Alizeti wanatarajiwa kunufaika na zao hilo kufuatia ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kukamua Alizeti kinachojulikana kama Mainland kinachojengwa katika eneo la Veyula, Jijini Dodoma ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji Desemba 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, amepata fursa ya kutembelea kiwanda hicho leo Septemba 06, 2024 na kujionea namna kilivyojipanga kuwainua wakulima wa zao hilo Mkoa wa Dodoma na hata mikoa jirani.
“Zao la alizeti ni la kimkakati kwa mikoa ya Kanda ya Kati hivyo kuona dhamira ya watu kutaka kuweka kiwanda kikubwa kama hiki ni jambo la fahari sana. Hamasa inatakiwa itolewe kwa wananchi wa Dodoma kwani sasa wana uhakika wa soko, wazalishe kwa uhakika kwani sasa wana mahali pakuuzia” Amesema Mhe. Senyamule.
Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa kiwanda hicho Bi. Betty Mkwasa, amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani 100 za mafuta yaliyochujwa kwa siku na kitahitaji tani 200 za malighafi kwa siku hivyo, ameiomba Serikali kuwapatia maeneo ya kuanzisha zao hilo kwa wingi.
Kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mainland, kinachojengwa na muwekezaji Mainland Group of Companies kutoka China, kinatarajiwa kuwa mkombozi kwa soko la Alizeti ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma pia kitazalisha ajira takribani 600 kwa wananchi.