Home BUSINESS JKT YASAINI MKATABA NA REA KUWEZESHA MRADI WA KUFUNGA MIFUMO YA NISHATI...

JKT YASAINI MKATABA NA REA KUWEZESHA MRADI WA KUFUNGA MIFUMO YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali SUMAJKT Brigedia Jenerali Petro Ngata wakionesha mkataba wa ushirikiano wa utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia mara baada kuusaini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali SUMAJKT Brigedia Jenerali Petro Ngata, akiipongeza REA kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati wa utiaji saini wa mikataba sita ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi za kupikia,hafla iliyofanyika leo Septemba 13,2024 jijini Dodoma.

Na.Mwandishi Wetu

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesaini mkataba wa kuwezesha mradi wa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika makambi 22 ya JKT katika mikoa 14 ambapo kati ya shiling bilioni 5.75 za mradi,Wakala wa Nishati Vijijini (REA) utachangia shiling bilioni 4.37 na kiasi kilichobaki Shiling bilioni 1.38 kitatoka JKT.
.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa mkataba huo leo Septemba 13,2024 Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT Brigedia Jenerali Petro Emmanuel Ngata (akimwakilisha Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele) amesema JKT ni miongoni mwa taasisi inayokwenda kufaidika na mpango huo wa serikali kupitia REA, JKT itaweza kupata vifaa bora na huduma mbalimbali zitakazowezesha JKT kuondokana na matumizi ya nishati haribifu ya kupikia katika makambi yake.
.
“Kwa kusainiwa mkataba leo, ni mwanzo wa Utekelezaji wa mradi katika makambi yetu ya JKT, mradi huu utakuwa ni suluhisho kwa Jeshi la Kujenga Taifa kupata nishati Safi ya kupikia ya uhakika kwa ajili ya Vijana wa JKT walioko makambini na pia kuondoa matumizi ya kuni kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwezesha kutunza mazingira yanayotuzunguka” alisema Brigedia Jenerali Ngata.
.
Aidha, Brigedia Jenerali Ngata amesema Jeshi la Kujenga Taifa limejipanga kuhakikisha linashirikiana na REA katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na unakuwa endelevu ili kuleta matokeo chanya ya malengo ya serikali na hivyo, makambi ya JKT kuendana na mpango mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here