Home LOCAL DKT.PHILIP AHIMIZA UWEKEZAJI UPANDIKIZAJI MIMBA KWA WATU WENYE CHANGAMOTO HOSPITALI YA MUHIMBILI

DKT.PHILIP AHIMIZA UWEKEZAJI UPANDIKIZAJI MIMBA KWA WATU WENYE CHANGAMOTO HOSPITALI YA MUHIMBILI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amehimiza uwekezaji uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wa Upandikizaji Mimba pamoja na uwashaji wa vifaa vya kusaidia kusikia kwa watu wenye changamoto ya kusikia kuwa endelevu.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya kuzindua Kituo cha Upandikizaji wa Mimba, kuwasha Vifaa vya Kusaidia Kusikia kwa Watoto na Kuzindua Gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Services) iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Amesema ni muhimu kuondokana na utegemezi wa wataalam kutoka nje na lazima jitihada za makusudi zichukuliwe ili kuwezesha uhamishaji wa teknolojia na ubunifu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati alipowasili Hospitali ya Taifa Muhimbili kwaajili ya kuzindua Kituo cha Upandikizaji wa Mimba pamoja na kuwasha Vifaa vya Kusaidia Kusikia kwa Watoto na Kuzindua Gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Service) tarehe 12 Septemba 2024.
Makamu wa Rais ameigiza Wizara ya Afya kuandaa mpango madhubuti wa kuwajengea uwezo wataalam wa ndani watakaoweza kuvitumia na kuvifanyia ukarabati vifaa vyote vya kisasa, pindi hitaji hilo litakapojitokeza.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema uzinduzi wa huduma za upandikizaji mimba na vifaa vya usikivu ni hatua muhimu sana katika kusaidia wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uzazi na watoto waliozaliwa wakiwa na changamoto ya usikivu. Amesema ni faraja kuona huduma ya upandikizaji wa mimba inaanza kutolewa kwa mara ya kwanza nchini katika Hospitali ya Umma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Services) la Hospitali ya Taifa Muhimbili katika hafla iliyofanyika hospitalini hapo tarehe 12 Septemba 2024.

Aidha ameongeza kwamba hatua ya kuboresha huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na upungufu wa wataalamu bobezi au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi ambapo imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, rufaa na kanda. Amesema Sambamba na uwekezaji mkubwa unaolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kibobezi, Serikali imedhamiria kutekeleza kwa vitendo ajenda ya kimkakati ya kukuza utalii wa tiba hapa nchini ili kuliongezea Taifa fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kupitia sekta ya huduma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Kituo cha Upandikizaji wa Mimba cha Dkt. Samia Suluhu Hassan kilichopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili katika hafla iliyofanyika hospitalini hapo tarehe 12 Septemba 2024.

Makamu wa Rais amempongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba, wataalamu na dawa, pamoja na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya. Amesema Serikali imeongeza Bajeti Wizara ya Afya kutoka Shilingi bilioni 900.1 mwaka 2020/21 hadi Shilingi trilioni 1.3 mwaka 2024/25 ambapo Katika kipindi hicho, fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya afya iliongezeka kutoka 40% ya bajeti ya afya mwaka 2020/21 hadi 59% mwaka 2023/24.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo ya namna ya upandikizaji mimba kutoka kwa Daktari Bingwa wa upandikizaji mimba Dkt. Chuor de Garang Alier wakati akikagua miundombinu ya Kituo cha Upandikizaji wa Mimba cha Dkt. Samia Suluhu Hassan kilichopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mara baada ya kuzindua kituo hicho tarehe 12 Septemba 2024.

Pia amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Aster DM Healthcare FCZ Bi. Alisha Moopen kwa kukabidhi Gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Service) kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo amesema uwepo wa gari hilo utasogeza huduma kwa jamii ambazo bado ziko mbali na vituo vya kutolea huduma lakini pia utasaidia kuboresha utoaji huduma za afya.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi zinazotoa huduma za afya nchini ili malengo ya serikali yaweze kutimia kwa ustawi wa wananchi. Amesema Wizara itajielekeza katika kushughulikia gharama za matibabu ya kibobezi ili kuwasaidia watanzania wote kuhudumiwa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na viongozi mbalimbali wakifurahi pamoja na mtoto Doreen Mtama mara baada ya kuwasha Kifaa cha Kusaidia Kusikia kwa mtoto huyo katika hafla iliyofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili tarehe 12 Septemba 2024.

Amesema Wizara itahakikisha wakati wa matumizi ya bima ya afya kwa wote kunakuwepo na mfumo wa rufaa utakaowezesha watanzania kufikia huduma kutoka tiba msingi hadi tiba bobezi.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika ambao utawezesha kusaidia watanzania wanaopitia changamoto za upatikanaji wa mimba pamoja na wale wenye changamoto ya kusikia.

Kuzinduliwa kwa Kituo cha Huduma ya Upandikizaji wa Mimba cha Hospitali ya Taifa Muhimbili kunaifanya hospitali hiyo kuwa ya kwanza kwa upande wa hospitali za umma kutoa huduma hiyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi, Wahudumu wa Afya na Wadau wa Sekta ya Afya wakati wa hafla ya kuzindua Kituo cha Upandikizaji wa Mimba, kuwasha Vifaa vya Kusaidia Kusikia kwa Watoto na Kuzindua Gari la Huduma Tembezi za Afya (Mobile Medical Service) iliyofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili tarehe 12 Septemba 2024.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
12 Septemba 2024
Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here