Home LOCAL DKT. BITEKO: RAIS SAMIA ANAAMINI KATIKA USHIRIKIANO NA VIONGOZI WA DINI

DKT. BITEKO: RAIS SAMIA ANAAMINI KATIKA USHIRIKIANO NA VIONGOZI WA DINI

*Atoa pole kwa Familia, KKKT kifo cha Askofu Sendoro

*Kanisa Lashauriwa Kumuenzi Askofu Sendoro kwa Vitendo

 *Waumini Waaswa Kuishi Maisha ya Kumpendeza Mungu

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na viongozi wa dini ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao ya kitume kwa maendeleo ya Watanzania.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 17, 2024 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mwanga, Kanisa Kuu lililopo Mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mara baada ya ibada ya mazishi ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Chediel Sendoro.

Askofu Sendoro amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Septemba 9, 2024 katika eneo la Kisangiro wilayani Mwanga.

“Rais yupo tayari kushirikiana na kanisa wakati wowote ili kanisa liweze kufanya kazi zote za kitume na sisi tuko tayari kuifanya Tanzania iwe bora na Watanzania waishi vizuri katika nchi yao,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa msingi wa Dayosisi hiyo umejengwa kwa upendo na kuwa moja ya kazi kwa viongozi wa kanisa hilo ni kupata mtu atakayeendeleza kazi na maono ya Askofu Sendoro juu ya kanisa hilo.

Amefafanua kuwa kila binaadamu ataiaga dunia itakapofika wakati wake ispokuwa kila mmoja aliyehai amefanya nini na hivyo hawana budi kukumbuka mahubiri ya Askofu Sendoro na umoja alioujenga miongoni mwao.

“Natoa pole kwa familia, wazazi, mjane, watoto na wajukuu kwa kuwa Septemba 9, 2024 lilitokea jambo lisilo la kawaida na kuondokewa na Askofu Sendoro. Nakupa pole Askofu Mkuu wa Kanisa, maaskofu wote na Wanamwanga, tuyaenzi yote aliyokuwa akiyaishi, alijali sana maadili yetu naomba tena tuendelee kuliombea Taifa na nchi yetu.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Rais Samia alishatoa muongozo na uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo juu hali ya siasa na vitendo vya uvunjifu wa amani nchini. “ Nataka niwaombe kama viongozi wa kiroho muendelee kushirikiana na Serikali kuwaombea Watanzania na kuifanya Tanzania kuwa mahali bora zaidi pakuishi.” Amemalizia Dkt. Biteko.

Akihubiri katika ibada hiyo Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Askofu Dkt. Alex Malasusa amesema kuwa siku ya leo ni siku ya pekee ambayo Askofu Sendoro amelala kwenye jeneza na kuwa ni jambo ambalo kibinadamu linatisha lakini hakuna kitakachoweza kuwatenga na tendo la Mungu.

“Hata katika hili Mungu anaonesha pendo lake, wazazi wake na watoto wake endeleeni kuamini Mungu ameonesha pendo lake, watu wa Mwanga mlikua na Askofu endeleeni kuliangalia pendo la Mungu msiliangalie hili gumu lililotokea angalieni pendo lake.” Amesema Askofu Malasusa.

Amesititiza “Nachotaka kukazia hapa kile tunachosema hasa sisi wachungaji kionekane katika maisha yetu, matendo yetu na kuishi kwetu. Mtakatifu Paulo anatufundisha kuwa yuko pamoja nasi, tuangalie alama ya msalaba ni alama ya ushindi.”

Aidha, Askofu Malasusa amewaeleza waombolezaji kuwa walio hai wanapaswa kuishi maisha ya uhakika ili Mungu atakapowaita wawe tayari na kuwa na ushuhuda wa kweli sio wa kusemwa na watu, na kuwa waendelee kuliombea kanisa.

Askofu Malasusa ametumia jukwaa hilo kuwataka Watanzania kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Aidha, amewataka viongozi wa kisiasa kukutana na kuzungumza juu ya changamoto zinazowakabili ili nchi iendelee kuwa na amani na mahali pazuri pa kuishi.

Akitoa salamu, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Cleopa Msuya amewataka wana Mwanga na KKKT kwa ujumla kumuenzi Askofu Sendoro kwa kuendeleza misingi imara aliyoijenga.

Amesema licha ya machungu waliyonayo waumini wanapaswa kujipanga na kupata viongozi watakaotimiza malengo yake juu ya kanisa hilo.

“Niombe watakaotafuta mbadala wake watupatie mtu ambaye yale yote aliyoanzisha yataendelea na kutuunganisha wakristo hapa Mwanga na Dayosisi zingine. Tafuteni mtu atakaye vaa viatu vya Askofu Sendoro.” Amesema Mzee Msuya.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tafayo amesema “ Nazungumza kwa niaba ya wananchi wa wote wa Mwanga kwa sababu yalipotokea matatizo mbalimbali Askofu Sendoro alishirikiana nasi watu wa Mwanga.”

Ameendelea kwa kusema kuwa Baba Askofu huyo aliwashirikisha waumini wa kanisa hilo katika shughuli mbalimbali wakati wa uongozi wake na kwa muenzi kwa wataendelea kushirikiana na uongozi wa Kanisa.

    

Share this Article

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here