Home BUSINESS BASHUNGWA ATOA ONYO KWA MAKAMPUNI YA UJENZI YANAYOBABAISHA WATEJA WAO.

BASHUNGWA ATOA ONYO KWA MAKAMPUNI YA UJENZI YANAYOBABAISHA WATEJA WAO.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amezinyoshea kidole baadhi ya Kampuni za Makandarasi Wazawa zinazoshindwa kutekeleza miradi na tenda za ujenzi wanazopewa kwa weledi na mujibu wa mikataba na kuanza kuwazungusha waliowapa kazi ambapo kitendo hicho kinaharibu taswira ya Makampuni ya Makandarasi wengine nchini.

Bashungwa ametoa onyo hilo, leo Septemba 04, 2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua Mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya mazingira katika utekelezaji wa miundombinu nchini.

Kuna Makandarasi mnaochukua zabuni za Ujenzi wa Majengo lakini baada ya kusaini mkataba, uswahili unaanza mpaka aliyekupa kazi anajiuliza hawa ndio Wazawa ambao Serikali inawatengenzea mazingira ya kuwapatia fursa mara dufu, sasa niwaombe kabla hatujachukua hatua mjirekebishe” amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameziagiza Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili ya Wakadiriaji Majenzi na Wabunifu wa Majengo (AQRB) kuanza kuchukua hatua baadhi ya Kampuni ya Makandarasi ya ujenzi yanayoshindwa kutekeleza kazi kwa weledi (Makanjanja).

Kadhalika, Bashungwa ameeleza kuwa dhamira ya Mheshimiwa Rais ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuwawezesha Makandarasi Wazawa ambapo tayari Wizara ya Ujenzi imesharekebisha masharti na kutoa fursa za ushiriki wa utekelezaji wa miradi kwa Wakandarasi nchini.

Bashungwa amewataka Makandarasi wanaofanya kazi za ujenzi wa majengo ya Serikali na Binafsi kutoyafumbia macho baadhi ya Makampuni yanayoharibu taswira ya taaluma yao na kuhakikisha wanalinda weledi na taaluma hiyo kwa kushirikiana.

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itaendelea kuhakikisha usimamizi wa ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara, madaraja pamoja na majengo yanaenda sambamba na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Sekta ya Ujenzi na Miundombnu Tanzania, Bw. Steven Mkomwa ameeleza kuwa mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali kuziangazia Sera, Sheria na Teknolojia zitakavyoweza kusaidia Sekta ya Ujenzi na kuweza kutoa mchango chanya katika masuala ya mazingira pamoja na uwepo wa miundombinu ya kijani.

Previous articleNAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MAENDELEO JAMII,JINSIA,WANAWAKE,NA MAKUNDI MAALUM AMEFUNGUA MAFUNZO YA SIKU MBILI
Next articleKAMATI YA NISHATI NA MADINI YATAKA KUONGEZA KASI UJENZI WA JENGO MAKAO MAKUU WIZARA YA MADINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here