Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali za Tanzania na Cuba zitaendelea kushirikiana katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo, Utalii na Masuala ya Teknolojia.
Ameeleza hayo baada ya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Mheshimiwa Salvador Valdes Mesa yaliyofanyika Revolutionary Square, Havana nchini Agosti 13, 2024.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko nchini Cuba kwa Ziara Maalum ya siku mbili kwa ajili ya kuboresha mahusiano baina ya Tanzania Cuba, amesema kuwa Wizara za Elimu za Tanzania na Cuba zinaendelea kutekeleza makubaliano ya muda mrefu ambapo Watanzania wengi wamesoma na wanaendelea kusomea udaktari nchini Cuba.
Aidha, ameeleza kuwa Wizara ya Afya Tanzania imekuwa ikiwaalika Madaktari Bingwa kutoka Cuba kuja Tanzania kushirikiana na Madaktari wa Kitanzania kutoa huduma ya matibabu ya kibingwa kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tumeshuhudia mara kadhaa Madaktari kutoka Cuba wakija Tanzania kufanya kazi katika hospitali kama vile Muhimbili, Mloganzila, Bugando, KCMC na Dodoma na wakati wote wamefanya kazi zao kwa bidii na uzalendo. Nimemuhakikishia Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa tuendelea kuuenzi ushirikiano huo wa kidugu”
Kuhusu Sekta ya Utalii, Waziri Mkuu amesema Tanzania inayo mengi ya kujifunza kutoka Cuba kwani nchi hiyo imefanikiwa sana kukuza utalii wa fukwe baada ya kuwa imejenga hoteli za kitalii, miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na kuwa na utaratibu mzuri wa magari ya kubeba watalii.
“Wacuba wanapokea watalii wengi sana, upo umuhimu mkubwa kwetu kujifunza mbinu wanazotumia kuvutia watalii wengi kutoka sehemu mabalimbali duniani.”
Vilevile katika kikao hicho, suala la kukuza lugha ya Kiswahili lilijadiliwa ambapo Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba ukiongozwa na Balozi Humphrey Polepole umejitwika jukumu la kusimamia mchakato mzima wa kufundisha na kuifanya lugha ya Kiswahili izungumzwe na kusambaa nchini Cuba na katika nchi za Latin Amerika.
“Hivi sasa Kiswahili kinafundishwa katika Vyuo Vikuu nchini Cuba na wanachuo wengi wanajitokeza kujifunza”
Naye Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amesema ziara ya Waziri Mkuu nchini Cuba imekusudia kukuza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kibayoyotekinolojia na katika maeneo ya taaluma kwa faida ya nchi mbili hizo.
Kuhusu Kiswahili, Balozi Polepole amesema kuwa Waziri Mkuu ameuelekeza ubalozi wa Tanzania nchini Cuba kuwa uendelee na maandalizi ya Kongamano la Kimataifa la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika Havana nchini Cuba Novemba 7-9, 2024. Mgeni rasmi katika Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.