Home LOCAL WATANZANIA  WASHAURIWA KUSAJILI WOSIA  RITA KUEPUKA MIGOGORO KATIKA FAMILIA 

WATANZANIA  WASHAURIWA KUSAJILI WOSIA  RITA KUEPUKA MIGOGORO KATIKA FAMILIA 

Na: Mwandishi wetu, Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya na Maofisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zote za mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kuhamasisha wananchi kuandika wosia ili kupunguza malalamiko na migogoro inayoweza kuepukika kwa warithi pindi wazazi au wategemewa wanapofariki.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi, na Udhamini (RITA) kwa wadau wa usajili katika mikoa hiyo, Kanali Sawala alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo zaidi watendaji hao katika huduma wanazotoa kwa wananchi ikiwemo mirathi, ndoa na talaka.

“Moja ya sababu kubwa ya migogoro inayotokea katika familia inasababishwa na baadhi ya wazazi kushindwa kuandika wosia kutokana na imani potofu ya kujitabiria vifo,” alisema Kanali Sawala na kuongeza kuwa kuuandika wosia sio kujitabiria kifo, kuna watu wengi walioandika wosia muda mrefu uliopita na bado wanaishi.

Aliwahimiza watumishi kutoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuandika wosia na kuwashauri na kuwasaidia namna ya kuandaa wosia huo ili kuepuka matatizo yanayoweza kuepukika katika jamii.

Aidha, Kanali Sawala aliwashauri wananchi kufanya kazi badala ya kutegemea mali za urithi ili wafaidike, hata kama wao siyo warithi halali kwani hiyo itasaidia kupunguza migogoro mingi isiyo ya lazima.

Mbali na kuipongeza RITA kwa hatua mbalimbali inazochukua ikiwemo kuwajengea uwezo watoa huduma, mkuu wa mkoa huyo alisema kuwa kuanzishwa kwa mfumo wa huduma kwa njia ya mtandao (eRITA) unaowawezesha wananchi kutuma maombi ya kwa njia ya kidijitali bila Kwenda Ofisi za RITA umeweza kunapanua wigo wa upatikanaji wa huduma na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Natoa rai kwa RITA kuweka nguvu zaidi katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutumia mfuma wa e-RITA kwani ni rahisi na unampunguzia mtu gharama ya kusafiri” alisisitiza Kanali Sawala.

Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw Frank Kanyusi, alisema taasisi yake imekuwa na utaratibu wa kuandaa mafunzo na vikao kwa wadau wa makundi mbalimbali ili kuwapa elimu na kujadiliana nao juu ya mikakati na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

“Mafunzo yaliyotolewa yaliwajengea uwezo watoa huduma wetu hasa katika maeneo ya usajili wa vizazi, vifo, ndoa, talaka, na udhamini,” alisema Bw. Kanyusi na kuongeza kuwa mafunzo yalilenga umuhimu wa takwimu ambazo ni kichocheo muhimu katika kupanga masuala ya uchumi kwa kutoa uhalisia wa mahitaji kwa wakati uliopo na kuwezesha kutoa makadirio ya mbeleni.

Bw Kanyusi alisema mafunzo hayo yametolewa kwa viongozi hao kwa sababu sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo inamtambua Katibu Tawala wa Wilaya kama Msajili wa Wilaya, hivyo wanahusika moja kwa moja na usajili wa vizazi, vifo, ndoa, pamoja na kufuatilia na kukusanya taarifa za hukumu za talaka katika maeneo yao.

Kwa upande wa Maofisa Ustawi wa Jamii, wao walipewa mafunzo hayo kwa sababu wao wanaratibu na kusimamia mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano.

Naye Mratibu wa Mpango wa Usajili wa Watoto chini ya Miaka mitano kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Bi. Mariam Nkumbwa, alisema kuwa kupitia mafunzo hayo yaliyotolewa na RITA, wanaamini zoezi la usajili na uingizaji taarifa kwenye mfumo wa usajili litaboresha na kufikia malengo waliyojiwekea.

“Kupitia mafunzo haya, tunategemea mikoa ya kusini kufanya vizuri katika usajili wa vizazi, vifo, ndoa, talaka, na udhamini,” alisema Bi. Nkumbwa.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala, Bw. Thomas Safari, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi kwani yatasaidia kuwafanya maofisa kufanya kazi zao kwa ufanisi kwa kufuata sheria, kanuni, na miongozo inayotolewa na RITA.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here