Home LOCAL WANANCHI WANAVYONUFAIKA NA MSAADA WA KISHERIA ZIARA YA RAIS SAMIA 

WANANCHI WANAVYONUFAIKA NA MSAADA WA KISHERIA ZIARA YA RAIS SAMIA 

Na: Mwandishi Wetu

TIMU ya wanasheria wa kampeni ya msaada wa kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid imeambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro kwaajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro iliyoanza tarehe mbili na inayotarajiwa kukamilika tarehe saba siku ya Jumatano mwezi huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema wameambatana na Rais Samia ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Tutakuwa na Rais muda wote wa ziara hapa Morogoro na tuko na Waziri wetu mheshimiwa Pindi Chana na wasaidizi wa kisheria ngazi ya wilaya na mkoa, kila anapofika mheshimiwa Rais kama kuna mtu anachangamoto ya kisheria tunaichukua na kuifanyia kazi,” alisema

“Kupitia ziara hii tumeshatoa msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali na hata jamii ya wamasai tumekutana nao kwenye maeneo mbalimbali na tumewapa elimu ya sheria kuhusu migogoro yao ya mara kwa mara ya ardhi,” alisema Beatrice.

Alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara hiyo, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legail Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya nane nane mkoani humo.

Beatrice alisema timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro juzi na inaendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi mbalimbali ambao wanamatatizo ya kisheia kwa kuwapa msaada wa kisheria.

Alisema tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya nane nane mkoani Korogoro wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la mama samia Legal Aid katika maonyesho hayoambapo wamekuwa wakipewa msaada wa kisheria.

Mama Samia yuko mkoani hapwa kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya za Mkoa wa Morogoro na mpaka sasa ameshatembelea Wilaya ya Gairo, Kilosa, Mvomero, na kesho Jumapili anatarajaiwa kuwasili wilaya ya Kilombero.

Mmoja wa wananchi aliyepata huduma ya msaada wa kisheria kwa mawakili na wanasheria wa Kampeni ya Mama Samia, Jerome Kiangi, alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kutatua matatizo yao ya kisheria.

“Kwa kweli nampongeza Rais Samia kwa upendo wake kwa watanzania amegundua kwamba wengi wetu tunahitaji msaada wa kisheria nimekuja hapa nimesikilizwa na wanasheria na wamesema tatizo langu la mgogoro wa nyumba litapatiwa ufumbuzi namshukuru sana,” alisema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, John Lubeja alipongeza hatua ya rais Samia kutuma wanasheria kwenye maonyesho hayo kwani wamekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria.

“Kupata wakili ni gharama sana kwa hiyo huduma kama hizi zinaposogezwa karibu na wananchi kama hapa kwenye maonyesho tena bure ni jambo la faraja sana na la kupongeza mno,” alisema Lubeja.

Hivi karibuni, Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, alisema kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid Campaign inatarajiwa kuanza kutikisa mikoa 19 kuanzia mwezi huu ili kuhakikisha wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha wanapata msaada wa kisheria.

Alisema kwenye mwaka wa fedha ulioisha walifanikiwa kuwafikia wananchi 500,000 na kwamba wameshapanga ratiba ya namna ya kuhakikisha wanaifikia mikoa yote iliyobaki.

“Tumeshapanga kila mwezi angalau tumalize mkoa mmoja kwa hiyo wananchi wawe na amani kwamba sisi tutawafikia kupitia kampeni hii mikoa yote ambayo hatujapita tutahakikisha tunapita mmoja baada ya mwingine,” alisema.

Alisema kwenye kampeni hiyo wanashirikiana na wadau mbalimbali kama Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania Bar Association.

Alisema mbali na wadau hao, mpango huo unafanyakazi kwa karibu na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia.

“Kwenye kampeni hii tumepata ushirikiano mkubwa sana wa mahakama, Jeshi la Magereza nao wamekuwa wakiratibu vizuri namna ya sisi kuwafikia wafungwa na mahabusu na kuwapa msaada wa kisheria na wadau wengine tunaomba tuendelea kusaidiana kufanikisha jukumu hili zito la kusaidia wananchi,” alisema.

Alisema pia wamekuwa wakifanyakazi kwa karibu na wasaidizi wa kisheria paralegals na aliwaomba kuendelea kushirikiana na serikali ili iwe rahisi kuwasogezea huduma za msaada wa sheria kwani wengi hawana uwezo wa kumudu kuweka mawakili kwenye mashauri yao. Aliwataka wasaidizi wa sheria ambao wako kwenye mikoa mbalimbali nchini wajitoe kwa nguvu zao zote kuwasaidia wananchi kwa kuwaandalia nyaraka za kuwasilisha mahakamani na kuwashauri namna ya kupata haki zao.

“Pia wahakikishe wanawapatia usuluhishi wa migogoro yao kwasababu kuna aina ya migogoro ambayo mnaweza kukaa nao mkazungumza na mkafikia mwafaka hata bila ya kufikishana mahakamani,” alisema

Alisema huduma hiyo ni endelevu na wasaidizi wa kisheria watakuwa wanapita kwenye mikoa mbalimbali hata ile ambayo wamepita kuwapa elimu wananchi kuhusu masuala ya kisheria.

Mama Samia Legal Aid Campain ilizinduliwa Aprili mwaka jana kwa kuanzia mkoa wa Dodoma na mpaka sasa tayari mikoa saba imefikiwa.

Mbali na Dodoma mikoa mingine iliyofikiwa ni, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga na Njombe na Ruvuma na kuanzia mwezi huu wanane wanatarajia kwenda kwenye mikoa mingine 19 awamu kwa awamu.

Mwisho

Previous articleNMB YAAHIDI NEEMA WADAU SEKTA YA KILIMO ILI KUNYANYUA UZALISHAJI 
Next articleKISHINDO CHA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA 88 DODOMA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here