Home BUSINESS WAKULIMA WA DENGU MANYARA WATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA SAHIHI ZA KUPOKELEA MALIPO YAO

WAKULIMA WA DENGU MANYARA WATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA SAHIHI ZA KUPOKELEA MALIPO YAO

Wakulima wa dengu wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Rift Valley (RIVACU LTD) Mkoani Manyara wametakiwa kuhakiki na kukabidhi taarifa zao za kupokelea fedha zikiwa hazina makosa kwa Makatibu wa Vyama vyao, ili kuepusha ucheleweshwaji wa malipo kwa wakulima ambao taarifa zao zina mapungufu.

Rai hiyo imetolewa na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Manyara, Absalom Cheliga, kwenye mnada wa nne wa zao la dengu uliofanyika katika ghala la Gendi.

Cheliga amesema kuwa wanunuzi wamekuwa wanalipa fedha za mnada kwa wakati na mkulima anapaswa kupokea fedha hizo ndani ya masaa 72 baada ya mnada kufanyika ila kumekuwa na changamoto ya kukosewa kwa taarifa za wakulima hali inayosababisha baadhi kuchelewa kupokea malipo.

Kwa upande wake Meneja wa RIVACU, Upendoel Valentine, amewaomba wakulima kuzingatia usafi na ubora ili waendelee kupata bei nzuri kwenye soko hilo la dengu.

Niwaombe Wakulima kuzingatia usafi na ubora wa dengu na niwatake muendelee kuleta dengu katika maghala kwani bei inayopatikana sokoni sasa hivi ni nzuri na tuache kuuza kwa walanguzi kwasababu tunapishana na bei iliyo nzuri kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani,” amesema Upendo.

Mkoani Manyara minada mitatu ya dengu imefanyika katika ghala la Endagaw wilaya ya Hanang, Gendi wilaya ya Babati na Maretadu wilaya ya Mbulu na wakulima wamekubali kuuza dengu hizo kwa Ghala la Endagaw Kilo 322,333 kwa bei ya wastani ya Shilingi 1,814, Ghala la Gendi Kilo 210,669, kwa bei ya wastani ya Shilingi 1,818 na Ghala la Maretadu Kilo 225,165 kwabei ya wastani ya Shilingi 1,756.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here