Chuo Kikuu Cha Dodoma wamefanya utafiti na kugundua tiba lishe ya kupunguza maradhi yasiyo ya kuambukizwa ikiwemo uzito uliopitiliza, shinikizo la juu la damu pamoja ugonjwa wa kisukari.
Akizungumza leo Agosti 4, 2024 katika Maonesho ya kimataifa ya kilimo Nanenane yanayofanyika Nzuguni jijini Dodoma, Mkufunzi Msaidizi wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) Bw. Kassim Ally, amesema kuwa tiba hiyo ni dawa ambayo inafanya kazi kwa ushirikiano kwa kula chakula kwampangilio wa kitaalam na kisayansi pamoja na kufanya mazoezi jambo ambalo litasaidia kupunguza magonjwa.
Amesema kuwa pia wamefanya utafiti wa kuongeza damu kwa ajili ya mama mjamzito wakati wa kijifungua kwani anakuwa anapoteza madini.
“Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma wamefanya utafiti na kuja na virutubisho
ambavyo vinaweza kupunguza changamoto ya maradhi ikiwemo kupunguza uzito” amesema Ally.
Amesema kuwa kuna maradhi mengi nchini yasio ya kuambukizwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuacha kutumia dawa kiholela.
Ameeleza kuwa ni muhimu watanzania wakafata wataalamu sahihi ambao wanatoa elimu kwa utaratibu na kuzingatia utaratibu kisayansi, huku akibainisha kuwa Chuo Kikuu Cha Dodoma kinatoa kozi ya Ushauri wa Tiba ya Lishe na Chakula.