Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeendelea na jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya matumizi sahihi ya Dawa na namna ya kuzihifadhi ili kujiepusha na madhara kwa kukosa elimu.
Elimu hiyo imetolewa na Mkaguzi wa Dawa mwandamizi Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya Kati Dodoma Benedict Brashi alipozungumza na wananchi waliotembelea Banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane-nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Brashi ameeleza kuwa ni muhimu wananchi kufahamu namna sahihi ya utumiaji na utunzaji wa Dawa, nakwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wamejihepusha na madhara yanayotokana na kushindwa kufuata maelekezo usahihi yanayotolewa na wataalamu.
Amesema kuwa kuna changamoto ya wagonjwa wengi kushindwa kumaliza dozi kwa wakati na hivyo kupata magonjwa sugu yanayosababisha matatizo makubwa kiafya.
“Kuna wagonjwa wengine wanapata dozi hospitalini lakini inafika mahali hizo Dawa hazitumii, na wengine wanagawana sasa ni muhimu wananchi waelewe kuwa ukipewa dozi ni ya mtu mmoja.
“sisi kama TMDA kuwasaidia wananchi namna ya matumizi sahihi ya Dawa ni jukumu letu kwaajili ya kuzilinda Afya zao na jamii yote kwa ujumla” amesema Brashi.
Amewataka wananchi wanaojihusisha na utengenezaji wa Dawa binafsi kuhakikisha zinapitia na kufanyiwa ukaguzi maalumu ili zithibitishwe na Serikali waweze kuuza kwa urahisi.
“Jambo muhimu hapa ni kuwa Dawa hizo zinatakiwa zichunguzwe kwa usahihi na kuona kama zinaleta matokeo yaliyotarajiwa kwa jamii”