Home LOCAL SERIKALI KUANDAA UTARATIBU WA KUTAMBUA MCHANGO WA VIJANA WANAOJITOLEA – NAIBU WAZIRI...

SERIKALI KUANDAA UTARATIBU WA KUTAMBUA MCHANGO WA VIJANA WANAOJITOLEA – NAIBU WAZIRI SANGU

Na. Lusungu Helela-Rukwa

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema Serikali inaandaa utaratibu rasmi
wa kutambua mchango wa vijana wanaojitolea kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali huku akiwataka vijana hao kuwa wavumilivu na wasikatishwe tamaa.

Amesema utaratibu huo utasaidia kupata watu sahihi wanaojitolea badala ya kupata mamluki ambao hupenyezwa na ndugu zao pindi fursa za ajira zinapojitokeza.

Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza katika mkutano ya hadhara uliofanyika katika Kata ya Ikozi na Kalambanzite zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipouteliwa kushika wadhifa huo.

Amesema udanganyifu huo umekuwa ukifanywa na baadhi ya Watumishi wasio waaminifu wenye ndugu zao na kupelekea manung’uniko kwa vijana sahihi wanaojitolea

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Sangu amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ipo katika hatua ya mwisho wa kuandaa utaratibu huo ambao utakuwa mwarobaini wa namna bora wa kutambua mchango wa vijana hao.

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na hivyo kupelekea baadhi ya watumishi ambao sio waaminifu kuanza kufuja fedha hizo

Kufuatia hatua hiyo Mhe. Sangu ameielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwabana watumishi hao ili kukomesha tabia hiyo.

Hata hivyo Mhe.Sangu amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuwasimamia watumishi wote nchini ili kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo zinapopelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo zinasimamiwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa

“TAKUKURU hakikisheni mnawabana watumishi ambao ni wadokozi wa fedha za miradi ya maendeleo inayotolewa na Rais wetu” amesisitiza Mhe. Sangu.

Previous articleSMZ IMEVUKA LENGO LA ILANI YA CCM KATIKA VIWANDA-DKT.MWINYI
Next articleMAFANIKIO MAKUBWA DAWASA, WAFIKISHA ASILIMIA 93 UTOAJI HUDUMA YA MAJIĀ 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here