Home LOCAL RC CHALAMILA ATAKA WAKAZI WA JIMBO LA UBUNGO KUUNGA MKONO JUHUDI ZA...

RC CHALAMILA ATAKA WAKAZI WA JIMBO LA UBUNGO KUUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI

-Asema Rais Samia ametoa pesa nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

-Atembelea na kukagua Soko la ndizi mabibo, ujenzi wa barabara KM 0.3 Makoka pamoja na kufanya mkutano wa hadhara Viwanja vya Shule ya Msingi mabibo Makuburi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila leo Agosti 14,2024 amefanya ziara katika jimbo la Ubungo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na Kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo ambapo amepata nafasi ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi papo hapo

RC Chalamila akiongea na wananchi kwa nyakati tofauti amewataka kuunga mkono juhudi za Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa maendeleo anayoyafanya yanaonekana katika maeneo mbalimbali ya Nchi hususani Wilaya ya Ubungo.

“Mhe Rais ametoa pesa nyingi katika Jimbo la ubungo ndiyo maana miradi mingi inatekelezwa” Alisema Chalamila.

Aidha RC Chalamila amekagua Soko la ndizi ambalo kwa muda mrefu lilikuwa halina faida kwa serikali lakini baada ya kurejeshwa mikononi mwa Halmashauri ya Ubungo sasa pesa zinaonekana na tayari maboresho ya soko hilo yameanza kufanyika.

Vilevile Mstahiki Meya Manispaa ya Ubungo Bw. Jaffary Juma Nyaigesha amesema Halmashauri inasimamia Soko hilo kwa weledi mkubwa ambapo amewaahidi wafanyabiashara wadogo wadogo wa soko la ndizi mabibo kuwa fedha zao zipo mikono salama na zitasaidia katika mikakati ya mpangilio sahihi wa sokoni tena wenye tija watu wengi.

Sanjari na hilo RC Chalamila alitembelea barabara ya Makoka ambapo aliwataka wakandarasi kukamilisha mradi huo kwa ubora,viwango na kwa wakati ili kuepusha athari zinazoweza kuletwa na mvua hapo baadaye.

Mwisho Wananchi wa Jimbo la Ubungo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe Hassan Bomboko walimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara yake na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maisha yao ambapo wamesema ziara hiyo imeacha matumaini mapya na ari ya maendeleo miongoni mwa wakazi wa Wilaya ya Ubungo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here