Na: Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezisisitiza taasisi na mashirika ya umma kuweka mikakati imara ili uwekezaji nje ya nchi uwe na tija kwa nchi.
Mhe. Rais Samia ameyasema hayo leo Agosti 28, 2024 jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha pili cha mwaka cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini.
“Uwekezaji nje ya nchi utakuwa na maana zaidi iwapo tutaonesha tija na ufanisi kwanza ndani ya nchi, hivyo nawasisitiza kujadili kwa mapana, kusikiliza uzoefu kwa waliofanikiwa na kutoa maoni ili baadae tuje na mikakati ya vipi tunakwenda kuwekeza nje ya nchi “, amesema Rais Samia.
Pia, amewasisitiza Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kujadili nafasi ya mashirika yasiyo ya kibiashara ambayo yana jukumu la kuwezesha sekta binafsi au mashirika mengine kufanya vizuri ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa, maono ya Mhe. Rais Samia ya kuifungua nchi yamekuwa msingi mzuri kwa nchi kwani baada ya miaka mitatu ya uongozi wake, nchi imeshuhudia kwa vitendo maana halisi ya kufungua nchi ikiwemo maendeleo katika sekta ya uwekezaji.
“Tunataka taasisi na mashirika ya umma nchini kuchangia kikamilifu katika kuifanya nchi ya Tanzania kuwa shindani na ndio maana tunaendelea kuzisukuma ili zijenge uwezo wa kuwekeza nchi za nje na kutoa huduma zenye hadhi na ubora wa kimataifa.” Amemalizia Prof. Mkumbo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya, Zakia Megji akizungumza kwa niaba ya Wenyeviti wa Bodi, amemuahidi Mhe. Rais Samia kuwa, daima wataendelea kumuunga mkono katika safari ya kufanya mabadiliko na kuendelea kuzisimamia taasisi na mashirika ya umma kwa juhudi ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanatimia.
Akieleza kuhusu kikao kazi hicho, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema kuwa kikao kazi hicho kitafanyika kwa muda wa siku tatu, kitajikita katika mada zinazohusu mikakati ya kupanua biashara au huduma nje ya Tanzania na kutumia vyema fursa zinazotuzunguka.
“Ili kupata uzoefu wa nchi zingine zilizopiga hatua katika uwekezaji na usimamizi wa mashirika ya umma, kikao kazi hiki kitakuwa na mada mahususi kutoka nchi zilizofanikiwa katika uwekezaji wa umma, pia tutapata uzoefu wa ndani kwa baadhi ya taasisi za ndani ya nchi zilizothubutu kuwekeza nje ya nchi ili kujenga uelewa wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuwekeza katika masoko ya nje”, amesema Mchechu.