Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Mhe. Raila Amolo Odinga, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) ikiwa ni mualiko kutoka kwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Dkt. William Samoei Ruto, Ikulu ya Nairobi, tarehe 27 Agosti, 2024.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inamuuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Raila Amolo Odinga anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU). Â
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati akishiriki uzinduzi wa kampeni ya kumnadi Mgombea huyo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Nairobi. Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Gervais Ndirakobuca na viongozi wengine.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Watanzania wanamfahamu Mhe. Odinga kama mwanamajumui wa Afrika anayeamini katika mtangamano wa Afrika na manufaa yake.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amempongeza Mhe. Odinga kwa kudumisha mahusiano mazuri na Viongozi wa Afrika na wabia wake.
Rais Dkt. Samia amemuelezea Mhe. Odinga kama kiongozi mwenye busara na mwenye uwezo wa kujenga Umoja wa Afrika thabiti, unayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya bara la Afrika na yenye uwezo wa kutetea maslahi ya Afrika kimataifa.
Sharifa B. Nyanga
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.