Home BUSINESS RAIS DKT. SAMIA KUFUNGUA RASMI KIKAO KAZI CHA MSAJILI WA HAZINA NA...

RAIS DKT. SAMIA KUFUNGUA RASMI KIKAO KAZI CHA MSAJILI WA HAZINA NA WAKUU WA TAASISI AGOSTI 28, 2024 JIJINI ARUSHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua rasmi kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali (CEO FORUM 2024), kitakachofanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2024, kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC Jijini Arusha.

Mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina una lengo la kuwaweka pamoja wakuu hao na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo maboresho yanayoendelea katika kuimarisha usimamizi, uendeshaji na utendaji wa Taasisi za umma sambamba na kubadilishana uzoefu.

Akizungumza na waandishi wa Habari Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda amesema kuwa kikao hicho kitafunguliwa rasmi Agosti 28, 2024, siku moja baada ya watendaji hao kuanza kukutana, nakwamba kinatarajiwa kufungwa rasmi Agosti 30 huu.

Aidha Mhe. Makonda, ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka kutumia ugeni huo kuweza kujinufaisha kupitia fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji.

Kikao kazi hicho ni cha pili baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza Mwezi Agosti 2023, ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma kuwekeza Nje ya Tanzania’ (‘Public and Statutory Corporations Business Strategies Beyond Tanzania’)

Kaulimbiu hii inalenga kuhimiza Taasisi na mashirika ya umma kuangalia fursa za kuwekeza au kupanua wigo wa Biashara nje ya Tanzania.

Aidha, Kaulimbiu hiyo inaunga mkono kauli ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Kikao Kazi cha mwaka jana 2023.

Katika Kikao hicho, Mhe. Rais alielekeza kuangalia uwezekano wa Mashirika kwenda kufanya Biashara au kupelekea huduma zake nje ya Tanzania.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia Taasisi na Mashirika ya Umma 304 Idadi hiyo inajumuisha Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chini ya asilimia 51.

Taasisi na Mashirika hayo yamekuwa na mchango muhimu katika kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali zikiwemo sekta za fedha, elimu, afya, hifadhi ya jamii, viwanda, biashara na kilimo.

Taasisi hizo pia zinachangia katika kukuza Pato la Taifa, kuchangia mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali, kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kukuza ajira, kurahisisha upatikanaji wa huduma na bidhaa, pamoja na kuhakikisha kuwa huduma na bidhaa zinazotolewa zinakuwa na ubora na bei stahiki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here