Home BUSINESS QATAR YAKARIBISHWA KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA FEDHA NCHINI

QATAR YAKARIBISHWA KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA FEDHA NCHINI

 

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amelikaribisha Taifa la Qatar kuwekeza katika sekta ya fedha nchini kwa lengo la kustawisha uchumi wa nchi zote mbili.

Gavana Tutuba ameyasema hayo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Taifa la Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi, katika ofisi za Makao Makuu ndogo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, tarehe 13 Agosti, 2024.

Amemueleza kuwa Tanzania ni mahali sahihi kwa ajili ya uwekezaji kwa sababu ina soko pana linalotokana na uwepo wa nchi hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) pamoja na makubaliano ya kuwa eneo huru la biashara la soko la pamoja Afrika (AfCFTA).

“Ukiwekeza Tanzania huwezi kujutia kwa sababu kwanza, imepakana na nchi zenye fursa mbalimbali za uwekezaji; pili, Tanzania ni mwananchama wa EAC na SADC, pia imeingia katika ya AfCFTA. Kwa hiyo, ukiwekeza Tanzania utapata fursa ya kuwekeza katika soko lenye takribani watu bilioni 1.5,” amesema Gavana Tutuba.

Ameongeza kuwa anafahamu kwamba Qatar ina mabenki yenye mitaji mikubwa na hivyo kukaribisha wawekezaji wa sekta hiyo kuwekeza Tanzania ili kuimarisha sekta ya fedha kwa nchi zote mbili.

“Nafahamu kwamba Qatar ina mabenki yenye mitaji mikubwa ambayo inaweza kuja kuwekeza Tanzania; tunawakaribisha kufanya hivyo na sisi Benki Kuu tumeweka mazingira rafiki ya benki hizo kushamiri hapa nchini,” amewaeleza.

Aidha, amesema kuwa uchumi wa Tanzania unazidi kuimarika kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Benki Kuu, ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei nchini.

Naye, Balozi Fahad Rashid Al Marekhi, ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Qatar kwa ajili ya kuchochea uwekezaji na biashara baina ya nchi hizo mbili. Pia, ameipongeza Benki Kuu kwa kusimamia vizuri uchumi wa nchi ambao unaifanya kuvutia wawekezaji nchini katika sekta mbalimbali.

    

Previous articleDCEA YAADHIMISHA SIKU YA VIJANA DUNIANI JIJINI ARUSHA
Next articleMAMLAKA YA AFYA YA MIMEA (TPHPA) YAOKOA TANI MILIONI 1.1 ZA NAFAKA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here